Dili La Dola Bilioni Nne

NYEMO CHILONGANI
DILI LA DOLA BILIONI 4

Sehemu ya Kumi na Moja.

Kwa Richard ulikuwa mtihani mgumu mno, hakuamini kusikia kauli kama ile kutoka kwa msichana aliyekuwa na sura mbaya kama Upendo akilazimisha kuwa naye kimapenzi.
Kwake lilikuwa suala gumu mno, hakuwa tayari kuwa na msichana huyo kwa kuwa hakumpenda, hakuwa mzuri wa sura na kitu ambacho kilimpa mawazo mengi ni kwa namna ambavyo watu wangegundua kama alikuwa akitoka na msichana huyo.
Alipendwa na mademu wakali, ambao walilala usiku na mchana huku wakimfikiria, alitongozwa na warembo mno na alijua kabisa kwamba angekuwa kwenye mapenzi na msichana huyo basi ingekuwa lazima kila mtu ajue kile kilichokuwa kikiendelea.
“Upendo! Kwani hakuna sharti jingine zaidi ya kuwa mpenzi wangu?” aliuliza Richard huku akimwangalia msichana huyo.
“Nilikuwa najiuliza swali linalofanana na lako, hivi hakuna mtu mwingine wa kumkopa pesa zaidi yangu?” naye Upendo aliuliza.
“Richard! Mbona ishu nyepesi sana hiyo! Kwanza mtoto wa kishua, utakula raha, yaani wewe tu! Halafu Upendo, hivi lile gari lako la Aston Martin si lipo?” alisema Robinson na kujifanya kumuuliza.
“Lipo!”
“Sasa je! Huo ndiyo muda wako kuendesha gari zuri! Piga mtoto huyu tupate hela tufanye biashara,” alisema Robinson huku akimwangalia Richard.
Ulikuwa ni mtihani mkubwa kwa Richard lakini hakuwa na jinsi kwa sababu tu msichana huyo ndiye alikuwa mtu pekee ambaye angewasaidia. Akakubaliana nao na hatimaye uhusiano ukaanza siku hiyohiyo.
Kwa Upendo ilionekana kuwa furaha kubwa, alikuwa pembeni ya Richard huku akionekana kuwa na furaha kubwa. Alimuhitaji mwanaume huyo, kwake, kila wakati alikuwa akitamani kuwaaminisha watu kwamba alikuwa mrembo na ndiyo maana alimchagua mwanaume aliyekuwa akitetemekewa na wanawake wengi chuoni hapo.
Watu waliomuona Upendo na Richard hawakuamini macho yao, ilionekana kama kituko fulani kilichojaa mshangao mkubwa. Hawakuamini kama yule mwanaume mzuri wa sura, aliyetetemekewa na kila mtu leo hii alikuwa na mtu kama Upendo.
Ubaya wa Upendo ndiyo uliowafanya wanaume wengi kumkimbia japokuwa alikuwa na pesa, hakukuwa na mtu aliyejua kilichokuwa kikiendelea, kwamba kila kitu kilichokuwa kikiendelea msichana huyo alikilipia kwa kuwakopesha kiasi kikubwa cha pesa.
Baada ya siku moja, Upendo akawakopesha vijana hao pesa walizokuwa wakizihitaji na hivyo kumuita Vonso na kuanza kuzungumza naye. Walimwambia kwamba muda ulifika, alitakiwa kuondoka nchini Tanzania na kwenda Marekani kwa ajili ya kusoma.
Barua ya kuomba nafasi iliandikwa, ilijibiwa na ni yeye tu ndiye ambaye alikuwa akisubiriwa. Baada ya kuongea na vijana hao, wakakubaliana na hatimaye akaanza safari ya kuelekea nchini Marekani kuanza masomo katika Chuo Kikuu cha Florida State kilichokuwa huko Tallahassee hukohuko Florida.
Kwenye kila kitu kilichokuwa kikiendelea kwake kilionekana kuwa kama ndoto, hakuamini kama vijana hao watatu, waliokuwa na umri kama wake ndiyo ambao walimsafirisha na kuelekea nchini humo.
Huko nchini Tanzania, vijana hao hawakutaka kuendelea kubaki chuoni, ilikuwa ni lazima waondoke na kwenda kutafuta maisha, hawakuona kama kulikuwa na umuhimu wa kuendelea na shule na wakati kulikuwa na michongo mingi ya kupiga pesa sehemu nyingine.
Walichokifanya ni kukutana na kupanga mikakati, wakakubaliana kuondoka kuelekea nchini Kenya, ilikuwa ni lazima wafanye kila liwezekanalo wapate pesa mpaka kufikia kiasi cha dola bilioni nne kama walivyokuwa wamepanga.
“Ila kwanza tuanzisheni akaunti yetu ambapo humo tutaweka milioni hamsini na kuendelea na ishu zetu,” alishauri Richard.
“Hakuna shida.”
Hilo ndilo walilolifanya, wakafungua akaunti na hatimaye kukiweka kiasi cha pesa walichotaka kikae humo na hivyo Robinson na Robert kuondoka kuelekea nchini Kenya huku wakimuacha Richard aendelee kula bata na mpenzi wake mpya.
Hawakutaka kufikia Nairobi, ili waanze kupata mambo mengi, kufanya mambo yao kwa uhuru ilikuwa ni lazima waelekee Mombasa kwanza. Wakaenda huko na kuanza kujipanga ni kitu gani walitakiwa kufanya.


Kenya ilivurugika, kila kona kulikuwa na maandamano yaliyokuwa yakimtaka waziri mkuu wa nchi hiyo, Bwana Osmon Kimeta kuachia ngazi kutokana na skendo nzito ya ubakaji iliyokuwa ikimkabili dhidi ya msichana mrembo, Jesca Ibrahim.
Kila mtu nchini humo alitaka kumuona waziri huyo akichukuliwa na kupelekwa mahakamani na kuhukumiwa kifungo cha miaka hamsini au zaidi.
Hakupendwa, kila kona alichukiwa kwa sababu ya ukaribu wake na Rais Andrew Kimoni. Wawili hao walikuwa marafiki kwa kipindi kirefu, walipanga mambo mengi, walifichiana siri nyingi mno huku wakiuhujumu uchumi wa nchi hiyo.
Katika kipindi hicho ambacho Kimeta alikuwa na kazi nzito ya kujisafisha ndicho kipindi ambacho Rais Kimoni alimwambia kuwa angemlinda na kusingekuwa na kesi yoyote ile mahakamani.
Viongozi kutoka katika vyama vya upinzani wakamtafuta Jesca, wakamuweka chini na kuanza kuzungumza naye, msichana huyo alikuwa na ushahidi wa picha ambazo alipiga na mwanaume huyo wakati akiwa anambaka, alifanya hivyo kwa kuwa hakuhitaji kufanya mapenzi.
Picha hizo zilikuwa kwenye barua pepe yake, nyingine akazihifadhi kwenye akaunti yake ya WhatsApp ya kulipia aliyokuwa akiitumia, yaani alihakikisha picha hizo zinahifadhiwa sehemu zote za siri ili iwe rahisi kwake kuwa na kumbukumbu ambazo angezitumia mahakamani.
Rais alimkingia kifua Kimeta, aliwaita mahakimu wote kwa siri na kuanza kuzungumza nao, aliwaonya kwamba kesi hiyo haikutakiwa kutoa hukumu kwa haki, kama kweli waliitaka kazi yao na kuendelea kuwa hai basi kwa yeyote ambaye angeisimamia ilikuwa ni lazima ampendelee Kimeta na kuonekana hata hatia yoyote ile.
Wakakubaliana, vitisho ambavyo walipewa viliwaogopesha. Huku nyuma viongozi wa vyama vya siasa waliendelea kumpampu Jesca aendelee kuisimamia kesi yake mpaka hukumu itakapitolewa.
Aliitwa mara nyingi na rais wa nchi hiyo na kumuomba sana akaifute kesi hiyo lakini Jesca hakukubali hata kidogo, tena aliongea kwa kujiamini kwamba ni lazima amfunge Kimeta ili iwe fundisho kwa watu wengine.
“Hii itakuwa fundisho kwa watu wengine,” alisema Jesca huku akionekana kujiamini.
“Ila usije baadaye kujutia uamuzi wako! Nakuahidi kama utafuta kesi, nitakupa shilingi milioni tano!” alisema rais huku akimwangalia msichana huyo.
“Huwa siongeki! Utupu wangu si wa kuuzwa kama malaya wa mitaani,” alisema msichana huyo.
Kila alipoitwa na rais aliongezewa dau lakini majibu yake yalikuwa yaleyale, hakutaka kukubaliana na rais huyo na alisisitiza kwamba ni lazima Kimeta afikishwe mahakamani na kufungwa kifungo kirefu.
Viongozi wa vyama pinzani walimlinda mno Jesca, walijua Rais Kimoni angefanya kila liwezekanalo kumuua msichana huyo, ili siku ya kesi ifike na hukumu itolewe ilikuwa ni lazima alindwe kwa nguvu zote.
Baada ya siku kadhaa kukatika hatimaye kesi ile ikapelekwa mahakamani, wananchi wote walifurahia, kwenye magazeti na mitandao ya kijamii kila mtu alimpongeza msichana huyo, alionekana kuwa shujaa kupita kawaida ambaye hakutaka kupokea pesa kutoka kwa rais, alichokiangalia ni kuangalia heshima ya utu wake.
Hatimaye jaji ambaye alitakiwa kusimamia kesi hiyo akatangazwa, kila mmoja alimjua mwanaume huyo, aliitwa Ibrahim Kifathi, ila alijulikana zaidi kwa jina la Nyoka.
Huyu alikuwa jaji pekee aliyeipendelea sana serikali, hata kuwe na kesi ya aina gani, hata kama serikali au mtumishi wa umma alifanya kosa la wazi, alipokuwa akisimamia, ilikuwa ni lazima mtu huyo ashinde.
Alichukiwa, kila kona alilalamikiwa lakini hakujali, alichokuwa akikiangalia ni maslahi yake tu. Mwanaume huyo ndiye ambaye alitakiw akuisimamia kesi hiyo kitu kilichompa ushindi mkubwa Kimeta.
“Hapana! Tunataka tubadilishiwe jaji!” kila mtu alilalamika lakini hakukuwa na aliyejali.
Siku zikaenda mbele, baada ya wiki moja hatimaye kesi ikaanza kusomwa. Watu walijazana mahakamani, kila mmoja alihitaji kusikia kilichokuwa kikiendelea, kesi ilikuwa inasomwa lakini kila mmoja alikuwa na hamu ya kutaka kujua zaidi kile ambacho kingetokea siku chache ambapo kesi hiyo ingeanza rasmi.
Wakati hayo yakiendelea ndiyo kipindi ambacho Robinson na Robert walifika nchini Kenya. Waliposikia kuhusu kesi hiyo, kitu ambacho kilikuja kichwani mwao kilikuwa ni pesa tu. Walifikiria pesa kuliko kitu chochote kile katika maisha yao.
Kwanza wakagongesheana mikono na kuambiana kwamba sasa kazi ilikuwa imekwisha, yaani walitaka kupiga pesa, wakaanza kufuatilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea.
Wakagundua kwamba kulikuwa na nafasi kubwa ya kupiga pesa. Kwanza kulingana na kesi yenyewe ilikuwa ni lazima kuwe na ushahidi wa picha ambazo msichana huyo alisema kwamba alikuwanazo.
“Kwanzahizo picha zitakuwa zimehifadhiwa kwenye barua pepe ama sehemu nyingine, sasa kama ni hivyo, ni lazima tufanye kila liwezekanalo kuzipata,” alisema Robinson.
“Haina shida. Kwa hiyo hapo pesa tutapiga kwa nani na nani?” aliuliza Robert.
“Daah! Yaani hapa kuna nafasi kubwa ya kupiga pesa mzee baba! Kwanza tutapiga pesa kwa huyu Jesca! Halafu tutapiga pesa kwa Kimeta, tutapiga pesa kwa rais Kimoni, halafu tutamcheki na huyu jaji anayesimamia, nitaangalia mafaili yake, naye pia tutapiga pesa kwake,” alisema Robinson huku akimwangalia Robert ambaye hakujua ni kwa namna gani wangepiga pesa hizo.
“Sijakuelewa mkuu!”
“Hahaha! Wewe subiri! Unataka tuanze kwa nani kupiga pesa?” aliuliza.
“Kwa jaji!”
“Hapana! Tuanze kwa Jesca. Atupe dola elfu hamsini!”
“Itakuwaje? Halafu inawezekana kweli akatupa? Inaonekana hana hela huyu!”
“Najua yeye hana pesa, ila watu waliokuwa nyuma yake wana pesa. Hawa viongozi wa vyama pinzani wana pesa sana, ngoja tuanze na yeye. Tukimalizana naye, tunaingia kwa Kimeta halafu rais, kisha jaji!” alisema Robinson.
“Basi sawa! Tuanze kazi!”
“Kazi hii inaanza na wewe mwenyewe!”
“Kivipi?”
“Utatakiwa kujifanya kuwa mwandishi wa habari kutoka Tanzania, omba kuonana na msichana huyu kwa ajili ya kumuhoji, kuwa na namba yake ya simu, wakati ukimuhoji, kuwa na laptop yako, fungua WhatsApp Web, halafu mimi nitaiingiza simu yake katika akaunti yake ya WhatsApp,” alisema Robinson.
“Sijakuelewa! Why WhatsApp?”
“Kwa sababu nilisikiliza mazungumzo yao kwa njia ya simu, msichana huyo alizihifadhi picha hizo kwenye akaunti ya WhatsApp, si unajua akaunti hizo watu wanashindwa kuzidukua, sasa mimi nitataka nitumie simu yake kuidukua,” alisema Robinson.
“Mh! Sawa.”
Huo ndiyo mpango uliopangwa, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kutengeneza kitambulishi ambacho kingemfanya Robert kuonekana kuwa mwandishi wa habari, haikuishia hapo, ilikuwa ni lazima pia watafute maiki na logo ambayo wangeiweka na kusomeka Mzalendo Tv ambayo ilikuwa moja ya kituo cha habari kikubwa nchini Tanzania.
Kila kitu kikakamilika na hivyo wote wawili kuanza safari ya kuelekea jijini Nairobi ambapo huko ndipo wangeanza kazi ya kumtafuta Jesca na kuzungumza naye. Ila jambo la kwanza kabisa walilotakiwa kulifanya ni kutafuta barua pepe yake, waingie humo na kuzifuta picha hizo kwanza, halafu wadili na zile ziliokuwa kwenye WhatsApp kitu ambacho kwao hawakuona kuwa kigumu kama tu wangetumia WhatsApp Web.

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumamosi ijayo.