I’M SORRY BASATA; 219 YA SUGU NI NGOMA KALI
Wiki iliyopita nilipata bahati ya kusikiliza ngoma mpya ya Sugu inayotambaa kwa jina 219. Niliposikiliza kigongo hicho, baadaye nikasikia Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), limeupiga ‘loki’ wimbo huo.
Nina mambo mawili ya kuzungumza; kwanza ni kuhusu wimbo na maudhui yake, pili ni Basata na uamuzi wake.
KUHUSU MAUDHUI
219 ni namba ya Sugu ambayo alipewa jela kama utambulisho wake. Kuhusu Sugu kuwa jela na sababu ya kufungwa siyo jambo lenye kuhitaji maelezo. Kila Mbongo anajua. Jumuiya za Kimataifa zinajua, wewe Mtanzania usijue kwa upofu na ukiziwi upi? Anyways, kama hujui muulize jirani yako, maana habari anayo!
Basi 219 Sugu amefanya ndio jina la wimbo. Ni ngoma kali. Credit kwa prodyuza Mr T Touch kwa uchakataji alioufanya ndani ya ‘kiwanda’ chake cha “Touchez Sound”, ila makofi mengi kwa Sugu a.k.a Jongwe kwa kazi nzuri; flaws zenye mamlaka ya kidingi kwenye game, ameitendea haki topic aliyoikusudia, kuhusu vina (rhymes), Baba Sasha-Desderia amenyoosha mbaya.
Bonge la chorus. “Mfungwa wa kisiasa 219, najua Mbeya ndio inanitesa. Lakini bado napenda Mbeya inavyonitesa.”
Ukiusikiliza wimbo unapata picha jinsi ambavyo Sugu alivyochukulia kifungo chake kwa tabasamu na kukigeuza mtaji kwa jamii yake ya Mbeya ambayo humwita Rais wa Mbeya. Mwaka 2020 ikiwa Sugu atagombea tena ubunge, hatatakiwa kuongea sana, akiweka tu mdude 219, anawarusha wapigakura, kura nyingi kwake.
Sijasikia tusi wala lugha yenye kuudhi kwenye wimbo. Je, labda ni aliposema wanataka kumshuti kama Lissu? Au alipohoji mbona Akwilina alipigwa risasi na kufa wakati hakusema chochote? Au alivyosema amefungwa bila kosa? Yaani kweli Basata walitaka Sugu afungwe halafu aseme alifungwa kihalali?
TUWAAMBIE BASATA
219 ni wimbo usio na kasoro yoyote. Tamko la Sugu kwamba atawapeleka mahakamani naliunga mkono. Mnafungiaje wimbo wa mtu ambao umekidhi vigezo vyote vya kisanii?
Basata mwache kutabirika. Wimbo hauna kasoro yoyote. Labda ni kutekekeleza agizo kutoka juu. Na hili Sugu amelisema kwenye wimbo: “mnamfunga mbunge bila kosa, matokeo yake wao ndio usingizi wanakosa.”
Sugu ni mwanamuziki. Hisia zake ataziweka kwenye muziki. Kama Papii Kocha alivyotoa “Waambie” baada ya kutoka jela au FM Academia ya Ndanda Kosovo walivyotoa Jela, ndivyo Sugu alivyotoa 219. Kumfunga ni sawa, lakini huwezi kumpangia namna ya kupokea na kuwasilisha hisia zake za kufungwa.
Poleni sana Basata. Mmepuyanga na uamuzi wenu. 219 ni wimbo wenye sanaa nzuri. Uvumilivu unahitajika katika kusikiliza yanayochoma.
Ndimi Luqman MALOTO