Kisa Cha Kweli:Kisiwa Cha Harishi

MTUNZI : FAKI A FAKI

Sikuwahi kuona sherehe kubwa ya harusi kama ile niliyoiona katika visiwa vya Ngazija nchini Comoro mwaka mmoja uliopita.
Ilikuwa harusi ya binti wa Rais wa Moroco Yasmini binti Sharif Abdilatif aliyekuwa akolewa na mwana wa mkuu wa majeshi ya ulinzi wa Comoro
Abubakar Mustafa Al- Shiraz aliyekuwa akiishi Ufaransa.
Sisi tulikuwa tumetoka Zanzibar. Mke wa mkuu wa majeshi ya Comoro Kulthum alikuwa Mzanzibari tena Mkojani wa Pemba, ndiye aliyetoa mwaliko kwa ndugu zake walioko Zanzibar.
Zilitolewa kadi kumi za mwaliko kwa watu kumi. Kwa vile na mimi nilikuwa na nasaba na Kulthum nikapata kadi moja na tiketi ya ndege ya kwenda Ngazija.
Wakati ule nilikuwa na umri wa miaka ishirini na minne(24). Nilikuwa bado kijana na shughuli zangu zilikuwa ni uvuvi. Nilikuwa sijaoa bado lakini nilikuwa katika maandalizi ya kutafuta mchumba.
Ndege tuliyosafiri nayo ilifika Comoro saa kumi jioni. Ndoa ilikuwa inafungwa saa mbili usiku baada ya swala ya Inshaa katika msikiti wa Riadha, msikiti mkuu wa Ijumaa nchini humo.
Nyumbani kwa bwana harusi kulikuwa kumejaa shamra shamra. Kadhalika nyumbani kwa Rais Sharif Abdulatif nako kulikuwa hakutoshi.
Kulikuwa na hoteli mbili kubwa zilizokodishwa siku ile kwa ajili ya sherehe za harusi. Na kulikuwa na hoteli nyingine kadhaa zilizokodiwa kwa ajili ya wageni walioalikwa kutoka nchi mbalimbali.
Sisi tulifikia katika hoteli ya Zaharani. Jina la hoteli hiyo lilifanana na jina langu. Jina langu ni Zaharani Shazume. Hoteli hiyo ilikuwa jirani na msikiti wa Riadha mahali ambapo ndoa ya Yasmin na Abubakar ingefungwa usiku ule.
Kwa kawaida msikiti wa ijumaa hujaa watu siku za ijumaa lakini siku ile kwa mara ya kwanza ulijaa watu katika swala ya Inshaa.
Kulikuwa na ulinzi mkali wa polisi na maafisa usalama waliokuwa na kazi ya kuhakikisha usalama unakuwepo katika eneo hilo.
Nilijitahidi sana nipate safu ya mbele lakini sikuweza. Safu hiyo ilikuwa imejaa masheikh na maafisa usalama. Nilibahatika kupata safu ya tatu yake.
Baadaya swala ya isha Rais wa Comoro Sharif Abdulatif alitakiwa kutoa idhini ya kumuozesha mwanawe.
Wakati anatoa idhini alipokea simu hapo hapo iliyomtambulisha kuwa binti yake Yasmin alikuwa ameanguka nyumbani na alikuwa akitokwa na povu mdomoni.
Shughuli ya ufungishaji ndoa ikasimama. Hapo hapo Rais Abdulatif na wasaidizi wake pamoja na maafisa usalama walitoka kwenda nyumbani.
Habari iliyopatikana baadaye ilieleza kuwa Yasmini alikuwa ameanguka na kupoteza fahamu huku akitokwa na povu midomoni. Baba yake alipofika na kumuona aliamrisha apelekwe hospitali haraka.
Gari la hospitali lilikuwa limeshafika. Yasmin alipakiwa na kukimbizwa hospitali. Gari hilo la hospitali lilifuatana na gari la maafisa usalama na gari la rais mwenyewe.
Lakini gari alilopakiwa Yasmin likapata ajali kabla ya kufika hospitali. Tairi lake la mbele la upande wa kulia lilipasuka na kusababisha gari hilo kuyumba na kuligonga gari jingine kabla ya kupindukia kwenye mtaro uliokuwa kando ya barabara.
Heka heka ikawa kubwa!. Magari ya maafisa usalama yakasimama. Maafisa hao wakashuka na kukimbilia kutoa msaada. Dereva wa gari la hospitali alipotolewa alikutwa akiwa ameshakufa. Yasmin mwenyewe hakuonekana. Wauguzi wawili waliokuwa naye walikutwa wamezirai. Tukio hilo lilizua taharuki kubwa.
Rais Abdulatif hakuamini macho yake, akawa anauliza kwa ukali “Binti yangu yuko wapi?”
Lakini hakukuwa na aliyejua. Yasmin alikuwa ametoweka ghafla. Kila aliyeshuhudia alishangaa.
Harusi ikavunjika. Badala ya furaha sasa ikawa huzuni. Bwana harusi na mke wa Rais Sharif Abdullatif Bi Kulthum
walikuwa wanalia kutokana na muujiza huo.
Usiku ule ule Rais Abdullatif aliita masheikh Ikulu na kuwauliza kama walikuwa wanajua kilichomtokea binti yake.
Kila sheikh alisema lake. Wako waliomwambia kuwa binti yake alikuwa amechukuliwa na wachawi. Wako waliomwambia kuwa haikuwa muafaka kwa binti yake kuolewa na Abubakar ndiyo sababu tukio hilo limetokea. Na wako waliomwambia kuwa Yasmin alikuwa amechukuliwa na jini aliyekuwa amemchunuka.
Rais Abdullatif hakujua ashike kauli ya sheikh yupi. Kwa vile lilikuwa limeshamfika alikubaliana na masheikh wote na kuwataka masheikh hao kutumia elimu zao kumrudisha binti yake. Aliahidi mamilioni ya shilingi za ki Comoro kwa sheikh yeyote atakayefanikiwa kumrudisha Yasmin.
Licha ya Rais Abdullatif kusubiri kwa zaidi ya miezi mitatu. Hakukuwa na sheikh yeyote aliyefanikiwa kumrudisha Yasmin! Yasmin akabaki kuwa historia kwani hakupatikana tena. Ulikuwa msiba ambao kila mkazi wa Comro alihisi kuwa hautasahaulika.
Hivi sasa mwaka mmoja umeshapita tangu tukio hilo la kuhuzunisha litokee. Tangu wakati ule sikuwahi tena kurudi Comoro. Nilikuwa Unguja nikiendelea na shughuli zangu za uvuvi.
Sasa siku moja ambayo sitaisahau maishani mwangu tulikuwa kwenye boti letu tukielekea maji makuu kuvua samaki. Ndani ya boti hilo tulikuwa wavuvi saba.
Ilipofika saa nne asubuhi tulikuwa mbali sana. Boti yetu ilipigwa na dharuba kali. Mashine ya boti ikazima ghafla. Tilijaribu kuiwasha lakini boti haikuwaka. Ikawa inakokotwa na maji.
Tulipumzika kidogo kisha tulijaribu kuiwasha tena na tena lakini hatukufanikiwa kuiwasha Mashine ilitugomea kabisa. Hatukujua ilikuwa imepatwa na hitilafu gani.
Je nini kitawatokea wavuvi hao?

Ngazija
Mkojani
Kulthum
Nasaba
Inshaa?

Naam Ustadh

SEHEMU YA 02

Hapo ndipo tulipoanza kufadhaika. Hatukuwa na la kufanya, tukawa tunatazamana!.
Tulikuwa tumepelekwa mbali sana kiasi kwamba hatukuweza kuona vyombo vyovyote ambavyo vingeweza kutusaidia. Tukakata tama kabisa.
Injini ya boti inapozima boti inakuwa kwenye hatari ya kupigwa na dharuba na kupinduka. Kama hilo lingetokea ungekuwa ndio mwisho wetu!
Hata hivyo bahari ilikuwa tulivu. Tatizo letu ni kuwa safari yetu haikuwa na mwisho wala muelekeo maalumu. Boti yetu ilikuwa inakokotwa kufuata upepo unakokwenda.
Mpaka jua linakuchwa hatukuwa tumetokea kwenye nchi yoyote wala kisiwa chochote. Ndani ya boti tulikuwa na vyakula vya akiba lakini hakukuwa na yeyote miongoni mwetu aliyesikia njaa.
Usiku ukapita kwa taabu huku tukiendelea kupelekwa. Asubuhi tuliendelea tena na jitihada ya kuiwasha injini lakini injini ilikataa katakata kuwaka. Tukaendelea kukokotwa hadi jioni. Hapo tukatoa vyakula vyetu na maji tukala kidogo tu.
Tulilala tena kwenye boti hadi siku ya tatu na ya nne. Vyakula vikatuishia licha ya kwamba tulikuwa hatuli sana. Tulibakisha maji kidogo tu.
Sasa tukahisi kwamba kama hatutakufa maji tutakufa kwa njaa kwani kwa siku hizo nne tulizokuwa baharini tulikuwa tumekonda.
Alfajiri ya kuamkia siku ya tano ndipo tulipotokea kwenye kisiwa. Sote tukashukuru ingawa hatukujua kilikuwa kisiwa gani na kilikuwa katika eneo gani.
Kilikuwa kisiwa kikubwa ingawa hakikuwa kikubwa sana. Kwa vile tulikitokea wakati wa usiku hatukukiona kwa sababu ya giza. Tulikiona kulipoanza kucha. Wakati tunakiona tulikuwa tumekikaribia sana. Sote tukapata furaha na matumaini ya kuokoka.
Mawimbi yaliendelea kutusukuma kidogodogo na kutufikisha kwenye maji madogo kabisa.
Suala kwamba kisiwa hicho kilikuwa kisiwa gani na kipo wapi halikuwa na umuhimu kwetu. Kilichokuwa muhimu ni kuwa tumefika mahali ambapo tungeweza kuyasalimisha maisha yetu nap engine kupata msaada wa kutuwezesha kurudi kwetu.
Tulishusha nanga na kushuka kwenye boti. Maji yalikuwa yakitufikia kwenye magoti. Tukaliacha boti na kutembea kwa miguu kwa kuyasukuma maji hadi tukafika ufukweni mwa bahari. Mahali tulipotokea hapakuwa na muinuko mkubwa. Tukapanda kwenye nchi kavu na kuanza kutembea kwemye vichaka huku tukiangaza macho huku na huku.
Kulikuwa na kunguru wengi waliokuwa wakiruka ruka kwenye miti. Jinsi walivyokuwa wakipiga kelele walikuwa kama wanaotukaribisha katika kisiwa hicho kilichokuwa kimya.
Tukaendelea kutembea tukiingia ndani zaidi ya kisiwa. Mtarajio yetu yalikuwa kupata mji au kijiji kilichokuwa kinakaa watu ili tuweze kusaidiwa.
Baada ya mwendo wa kama nusu saa tulianza kuona vibanda vilivyokuwa vimebomoka. Tukapata matumaini kuwa kulikuwa na watu waliokuwa wanaishi katika kisiwa hicho. Pia tulikuta visima viwili vya maji ambavyo vilikuwa vimekauka.
Wakati tunaendelea kwenda ghafla tuliona tumetokea kwenye barabara pana ya changarawe. Tukaifuata ile barabara mpaka tukatokea katikati ya mji. Ulikuwa mji mzuri uliokuwa na barabara na majumba. Lakini nyumba zote zilikuwa zimechakaa na kubomoka. Baadhi yake zilionekana kama mahame.
Jambo ambalo lilitushangaza ni kuwa hatukuona mtu hata mmoja. Mji wote ulikuwa kimya kabisa. Tulikuwa ni sisi peke yetu tu. Tulikatiza mtaa hadi mtaa kutafuta wenyeji wa kisiwa hicho lakini hatukuona mtu.
Udadisi ukatufanya tuanze kuingia katika zile nyumba. Tuliingia katika
nyumba ya kwanza. Tukakuta vitu vya ndani vilivyochakaa na kukongoroka. Vilikuwa kama vitu vya zamani visivyotumika tena. Katika kutafiti tafiti tulishituka tulipokuta mafumvu na mifupa ya binaadamu. Kuna iliyokuwa imelala kwenye kitanda na mengine ilisambaa ovyo.
Tukatoka haraka katika nyumba ile na kuingia katika nyumba nyingine, nako tulikuta vitu mbalimbali vya ndani ya nyumba vilivyokuwa vimechakaa na mifupa ya binaadamu.
Tukawa tunatazamana kwa hofu. Kila mmoja wetu alikuwa akijiuliza moyoni mwake, kulikoni? Lakini hatukupata jibu.
Katika mitaa mengine tulikuta mafuvu na mifupa ya binaadamu ikiwa barazani mwa nyumba na kando kando ya barabara. Tulivyozidi tena kwenda mbele tulikuta mifupa ya mikono nay a miguu ya binaadamu ikining’nia kwenye miti. Tukawa tunazidi kuitazama ile mifupa huku tunazidi kwenda.
Ghafla tukatokea kwenye jumba moja kubwa. Jumba hilo ndilo lililokuwa kubwa na zuri kuliko jumba lolote katika kisiwa hicho.
Mbele ya jumba hilo kulikuwa na bustani ya maua na miti ya vivuli. Kutokana na uzuri wa jumba hilo tukaona tuingie ndani ili tuangalie lilivyo.
Tulipoingia tu pua zetu zilikaribishwa na harufu nzuri ya manukato yaliyokuwa yananukia humo ndani. Tulitembea katika sakafu ya marumaru iliyonakishiwa maua ya kupendeza.
Tulikuwa tumeingia katika ukumbi mpana uliokuwa na madirisha na mapazia ya hariri. Tulikuta meza, viti na makabati. Zilikuwa fanicha za kifahari sana.
Baada ya kuupita ukumbi huo tulitokea katika kumbi nyingine ndogondogo zilizokuwa na vyumba vipana. Tukawa tunaingia kila chumba kuchunguza.
Katika chumba cha kwanza tulikuta kitanda kilichotandikwa vizurii. Pia tulikuta makabati ya vioo yaliyokuwa yanapendeza.
“Inaelekea kuna watu wanaoishi ndani ya jumba hili” Mwenzetu mmoja akasema.
“Lakini mbona hatuwaoni hao watu?” Mwingine akauliza.
“Ndiyo hatuelewi sasa” aliyesema mwanzo akamjibu.
Je wavuvi hao wametokea kwenye kisiwa gani hicho na ni kitu gani kitakachowatokea?

Endelea

SEHEMU YA 03

Tulitoka katika kile chumba tukaingia katika chumba kingine. Pia tulikuta kitanda na makabati. Tukawa tunatazamana kwa mshangao. Kutoka hapo tulichangukana. Kila mmoja akawa anafungua chumba alichotaka na kuangalia ndani.
Mimi niliingia katika vyumba viwili. Nilipoingia chumba cha tatu nilishituka nilipomuona msichana mzuri amelala kitandani. Alikuwa amelala usingizi kabisa huku amejifinika shuka kuanzia miguuni hadi shingoni. Uso wake uliokuwa wazi ulikuwa umeelekea upande wangu.
Nilipomuona nilisita kwenye mlango na kujiuliza msichana huyo ni nani na kwanini alikuwa peke yake katika jumba hilo.
Baada ya kusita kidogo niliingia ndani. Nilikuwa nataka kuhakikisha kama alikuwa hai kweli au amekufa.
Nilipofika karibu yake, msichana huyo alifumbua macho ghafla. Akashituka aliponiona.
“Wewe nani?” akaniuliza kwa mshangao akitumia lugha ya kingazija ambayo nilikuwa siijui vizuri. Lakini nilimjibu kwa Kiswahili.
“Mimi ni mgeni katika kisiwa hiki na katika jumba hili, je wewe ni nani?”
Alikuwa anajua Kiswahili. Akanijibu kwa Kiswahili cha kipemba.
“Miye ni Yasmin, binti wa Rais Shariff Abdilatif wa Comoro!”
SASA ENDELEA
Nilishituka sana aliponiambia yeye ni binti wa Sharif Abdulatif wa Comoro.
Papo hapo nikakumbuka ile harusi iliyovunjika kati ya binti wa rais wa Comoro na mwana wa mkuu wa majeshi ya ulinzi nchini humo.
Mimi nilikuwa mmoja wa waalikwa kutoka Zanzibar na nikashuhudia maajabu. Yasmin alitoweka katika mazingira ya kutatanisha baada ya gari iliyokuwa inampeleka hospitali kupasuka tairi na kuingia kwenyenye mtaro. Yasmin alikuwa anakimbizwa hospitali baada ya kuanguka ghafla wakati baba yake Rais Sharif Abdulatif anataka kutoa idhini ya kumuozesha binti yake.
Baada ya kutoweka ghafla kwenye gari, Yasmin hakupatikana tena na sasa mwaka ulikuwa umeshapita.
Ingawa sikuwahi kuonana naye uso kwa uso lakini niliona picha zake katika magazeti na televisheni wakati habari zake zilipokuwa zinaandikwa na kutangazwa.
Alikuwa ndiye Yasmin kweli binti wa Rais Sharif Abdulatif wa Comoro.
Kwa kweli tukio la kumkuta ndani ya jumba hilo na katika kisiwa kile kisicho na watu, mbali ya kunishitua, liliniongezea hofu mara dufu.
“Wewe ni binti wa Rais wa Comoro” nikamuuliza kwa mshangao.
Huku akinyanyuka kwenye kitanda na kuketi msichana huyo alinijibu.
“Ndiye mimi. Rais Sharif Abdulatif ni baba yangu”
Nikiwa kwenye mshangao niliendelea kumtazama msichana huyo bila kummaliza. Alikuwa amevaa shumizi inayoonya. Alipoketi alijifunga ile shuka kwenye mwili wake kama mtu aliyekuwa anaona baridi. Lakini nilijua alikuwa anajisitiri kwa sababu sumizi aliyovaa ilikuwa inaonya.
Kwa tamaduni za kiislamu na za kule Comoro mwanamke hatakiwi kuonekana mwili wake pamoja na kichwa chake.
Lakini Yasmin kwa sababu ya kutaharuki alisahau kujifinika kichwa. Nywele zake za mawimbi zilizokuwa ndefu zilikuwa zimeshuka na kumfikia mabegani.
“Yasmin umefikaje huku?” nikamuuliza.
Yasmin akanitazama. Macho yake makubwa yenye mboni za rangi ya kahawia yalinifanya nikiri kimoyomoyo kuwa Yasmin alikuwa mzuri.
Badala ya Yasmin kunijibu, na yeye akaniuliza.
“Kwani wewe umefikaje hapa?”
“Mimi siko peke yangu, nina wenzangu na tumefika hapa kwa bahati mbaya. Sisi ni wavuvi kutoka Zanzibar. Chombo chetu kilipigwa na dharuba kikapata hitilafu. Kwa siku nne kilikuwa kinaelea kwenye maji, hatujui tunakokwenda. Leo siku ya tano ndio tumetokea kwenye kisiwa hiki”
“Huko ulikopita hadi umetokea hapa, umeona nini?”
“Tumekuta nyumba hazina watu. Pia tumekuta mafuvu na mifupa ya watu kila mahali”
“Basin a nyinyi ndio mtakuwa hivyo hivyo, hamtapona”
Yale maneno yalinitisha na kunifadhaisha.
“Yasmini kwanini unaniambia hivyo. Mimi ni ndugu yako wa Zanzibar. Hata katika harusi yako na mwana wa mkuu wa majeshi ya ulinzi wa Moroco nilialikwa na nilikuja Comoro lakini wewe ulitoweka katika mazingira ya ajabu. Na leo ndio nakuona hapa” nikamwambia Yasmin kwa hofu.
“Nashukuru kwamba leo nimetembelewa na ndugu yangu wa Zanzibar na nashukuru kwamba umenijua lakini naona uchungu kuwa nitayashuhudia mauti yako muda si mrefu”

Kwanini unaniambia hivyo Yasmin?. Niambie”
Yasmin bdala ya kunijibu aliangua kilio.
Wenzangu mmoja mmoja wakaanza kuingia mle chumbani na kushangaa kumuona yule msichana akilia.
“Je ni nani huyu?” Mmoja wa wale wenzangu akaniuliza wakati wenzetu wengine walikuwa wamepigwa na butwaa.
“Ni msichana nimemkuta amelala humu chumbani. Nilipoingia alizinduka na kuniambia anaitwa Yasmin. Ni binti wa Rais wa Comoro” nikawaeleza.
“Ni binti wa Rais wa Comoro?” Baadhi ya wenzangu wakaniuliza kwa mshangao. Walidhani labda nilikosea kusema.
“Ndiyo, mwenyewe ameniambia hivyo na mimi pia namfahamu. Nilihudhuria katika harusi yake nchini Comoro mwaka uliopita.
“Si ilisemekana kuwa yule binti alitoweka?” Mmoja wa wenzangu akauliza.
“Ni kweli. Mimi pia nimeshangaa kumkuta katika kisiwa hiki, tena akiwa peke yake. Na amenieleza kitu cha kutisha”
“Kitu gani?”
“Mh! Ameniambia anaona uchungu kuwa atayashuhudia mauti yetu muda si mrefu!”
Wenzangu wote wakashituka, ndipo nilipojua kuwa hakuna mtu anayependa kufa.
“Kwanini amekwambia hivyo?” Sautu za kuuliza zilisikika kutoka kwa wenzangu.
“Ndio nilikuwa namuuliza, naona analia”
“Asilie, atueleze ili tujue…”
“Usilie dada yangu, nyamaza utueleze ili tujue jinsi ya kujihami” nikamwambia msichan huyo.
“Pia atueleze jinsi alivyofika katika kisiwa hiki cha ajabu” Mtu mwingine akasema.

Nashusha nondo faster faster

SEHEMU YA 04

ILIPOISHIA
Yasmin akajifuta machozi yake kwa shuka aliyokuwa amejifunga kisha akainua uso wake na kututazama. Sasa macho yake yalikuwa mekundu na uso wake ulikuwa umeiva.
“Wiki moja kabla ya harusi yangu huko Comoro nilikiota hiki kisiwa. Nikamuota kichaa mmoja akiniambia siku zako zimekaribia za kuja kukaa katika kisiwa hiki” Yasmin akaanza kutueleza. Tukawa tunamsikiliza kwa makini.
Akaendelea. “Nikamwambia yule kichaa, siwezi kuja kukaa hapa, mimi natarajia kufunga ndoa hivi karibuni. Nitakwenda kukaa Ufaransa si hapa
“Yule kichaa akaniambia, ndoa yangu nitafunga na yeye kwani yeye alinichunuka tangu nilipokuwa ninasoma na hatakubali niolewe na mtu mwingine.
“Nilipoamka asubuhi nilipuuza ile ndoto. Sikumuelezea mtu yeyote na kwa kweli nilifanya kosa kuipuuza, pengine nisingekuwa hapa leo hii. Yaani mpaka leo hii ninajuta”
Msichana huyo akaendelea kutuelea. “Ile siku ya harusi yangu ilipofika saa mbili usiku niliona kizunguzungu. Macho yangu yakafunga kiza. Nikaona kama moyo wangu unanisokota na ghafla nikapiga ukelele na kuanguka chini. Baada ya hapo sikujijua tena
“Nilizinduka asubuhi na kujikuta nomo ndani ya jumba hili katika kisiwa hiki. Mbele yangu nikamuona yule kichaa niliyemuota akiniambia kuwa nitakuja kukaa hapa”
SASA ENDELEA
“Yule mtu niliyemuota hakuwa binaadamu bali alikuwa jinni aliyekuwa amenichunuka. Siku ile nilipomuota nilimuona katika sura ya kibinaadamu kichaa lakini nilipozinduka nikiwa katika jumba hili alikuwa katika sura na umbile la kijini” Yasmin aliendelea kutueleza. Kisa chake kilikuwa kimetushangaza na kutuogopesha.
Akaendelea. “Huyo jinni aliponiona nimeshituka aliniambia Yasmin usiogope umeshafika nyumbani kwako, mimi ndio nitakuwa mume wako. Utaishi katika jumba hili na hutarudi tena kwenu.
“Akaniambia kwamba yeye ni jini wa ukoo wa kisubiani makata. Jina lake ni Harishi wa Harishn. Chakula chake ni damu ya binaadamu. Ameniambia wazi kuwa yeye ni jini mbaya aliyelaaniwa na ameshaua watu wengi.
“Akanihadithia kisa cha kisiwa hiki. Aliniambia kilikuwa kinaishi watu zamani na mfalme wao alikuwa akiishi katika jumba hili. Lakini yeye harishi ndiye aliyewaua mmoja mmoja kwa kuwafyonza damu hadi kukimaliza kisiwa chote.
“Watu wachache waliobaki waliondoka na kikiacha kisiwa kikiwa kitupu. Ndiyo sababu mlikuta magofu matupu na mifupa ya watu waliouliwa na Harishi. Siku za mwanzo mwannzo mji huu ulikuwa haukaliki kwa harufu zilizotokana na maiti za watu. Kunguru wa Zanzibar walihamia hapa kujipatia riziki zao. Sasa hivi iliyobaki ni mifupa mitupu.
“Kwa sasa kisiwa hiki kinajulikana kama kisiwa cha mauti. Wavuvi ambao hawajui habari za kisiwa hiki wakifika hapa kushona nyavu zao Harishi aliwaua mmoja mmoja kwa kuwafyonza damu”
Maelezo ya Yasmin yalitufanya tutazamane mara kwa mara huku nyuso zetu zikiwa zimepigwa na butwaa. Hatukuwahi kusikia kisa cha ajabu kama kile.
“Mimi nilikuwa nikilia peke yangu hadi sasa silii tena. Ni kama nimeshazoea kuishi na yule jinni” Yasmin aliendelea kutueleza.
“Kila wiki ankuja mara moja. Au kama nina dharura ninamuita, anakuja. Humu ndani mna kila kitu. Mna kila aina ya vyakula. Huwa najipikia mwenyewe chakula ninachotaka. Vyakula vikipungua ananilete vingine.
“Pia ananiletea nguo za kifalme pamoja na dhahabu. Huwa anaiba nguo hizo katika kasri za wafalme na marais. Kila kitu ninachotaka ananiletea lakini hainisaidii. Maisha ya upweke yananifanya nijione kama nimo ndani ya kaburi”
Wakati Yasmin anatuhadithia kile kisa, nilimuuliza. “Umetuambia huyo jini anafyonza damu za watu na kuwaua, je wewe utaendelea kuwa salama kweli”
“Mimi nimeshakuwa mke wake. Ameniambia damu yangu ni haramu kwake. Hawezi kuniua ila hatanirudisha tena kwetu. Nitaendelea kuishi hapa hadi mauti yanikute” Yasmin alituambia.
Kwa kweli hayakuwa maneno ya kuogopesha tu bali pia yalikuwa yanasikitisha sana.
Maisha ya Yasmin yalikuwa yanasikitisha. Alionesha wazi kukata tama na pia niliona kwa vyovyote itakavyokuwa maish yake yatakuwa mafupi.
“Kwa hiyo sisi hatutapona?” Mwenzetu mmoja akamuuliza Yasmin
“Sipendi niwafiche, nawaeleza ukweli ili mujue kuwasaa zenu zimekaribia sana”
“Je kama tutaondoka ndani ya jumba hili na kwenda kujificha mahali pengine?”
“Mtajificha wapi ambapo hafiki. Kisiwa chote hiki amekimiliki yeye. Halafu yeye ni jini, lazima atawagundua tu”
“Sisi tuko watu saba. Kweli ataweza kutuua sisi sote kwa pamoja?”
“Nyinyi atawaua mmoaja mmoja. Leo akiua mmoja, kesho anarudi tena kuua mwingine hadi mtamalizika nyote. Akishaua mtu anamtupa nje aliwe na kunguru”
Msichana akatikisa kichwa peke yake kabla ya kuendelea.
“Halafu hataki kuona mtu humu ndani. Wivu wake ni mkali sana. Siku nyingine anakuja na hasira, anasema anasikia harufu ya mtu humu ndani, basi hunipiga hadi nazimia kisha huenda zake”
Kila mmoja wetu aliguna na kumtazama mwenzake.
“Unadhani atakuja lini tena?” nikamuuliza.
Usipitwe na Uhondo huu
ITAENDELEA

SEHEMU YA 05

“Sasa unamuitaje?”
“Alinipa chupa. Mnaiona ile chupa iliyopo juu ya kabati? Chupa ile iko wazi. Kifiniko chake kipo pembeni. Ameniambia nisiifunge. Anapotaka kuja ile chupa inajaa moshi halafu inavuma. Ule moshi ukishajaa unatoka kwenye mdomo wa ile chupa na kuundaumbile la jinni halafu anakuwa jinni kabisa.
“Sasa nikitaka kumuita nachukua ile chupa naiweka naiweka karibu na mdomo wangu kisha nataja jina lake mara tatu, hazitapita dakika mbili chupa itajaa moshi. Moshi ule utatoka kwenye mdomo wa chupa na kugeuka Harishi”
“Sasa kama anakuja kila wiki tutapata muda wa kuishi na pengine tunaweza kupata msaada kwani tutakwenda kukaa fukweni kusubiri vyombo vinavyopita” nikamwambia Yasmin
“Jaribuni hahati yenu. Nawaombe Mungu awasalimishe” Yasmin alituambia kwa ungonge.
Nikawambia wenzangu. “Jamani maneno mmeyasikia. Hapa hapakaliki”
“Sasa tuondoke” Mtu mmoja akauliza.
“Inabidi tuondoke tusalimishe maisha yetu”
“Sasa tutakwenda wapi?” Mwingine akauliza.
“Twende ufukweni tuangalie vyombo vinavyopita, tunaweza kupata msaada”
“Sasa huyu msichana naye
tumchukue?” Mtu mwingine naye akauliza.
SASA ENDELEA
“Itakuwa ni jambo zuri tukimchukua kama mwenyewe atakubali” nikawambia wenzangu kish nikamtazama Yasmin.
“Bibie unaonaje kama tutakuchukua ili tukunusuru?” nikamuuliza yasmin.
“Kunichukua mimi hakutakuwa nusura kwangu wala kwenu kwa sababu mpaka sasa hamna uhakika wa usalama wenu hata kama mtakwenda ufukweni mwa bahari kusuiri vyombo vinavyopita” Yasmin akatuambia.
“Kwanini unatuambia hivyo?” nikamuuliza.
“Kwa sababu Harishi anaweza kututoke hapa hapa na kutuua sote kwa hasira’
Sote tukagunana kutazamana. Yasmin aliendelea kutuambia.
“kwanza akija hapa nyumbani hata kama mtakuwa mmeshaondoka atasema anasikia harufu ya binaadamu na atataka kujua ni nani aliyeingia humu na itakuwa ni balaa kubwa”
“Sasa unatushauri nini?” nikamuuliza Yasmin katika hali ya kukata tama.
“Nawashauri muondoke ndani ya jumba hili. Mwende popote mtakapoona mtaweza kujiokoa. Mimi niacheni hapa hapa”
“Sawa. Basi sisi tunondoka”
Yule msichana kwa kuonesha wema na ukarimu alituambia tumpishe mle chumbani avae nguo. Tukatoka ukumbini. Yasmin alipovaa alitoka akaenda jikoni. Akachukua vyakula na kututilia ndani ya mfuko.
“Sasa nendeni, msikae karibu kabisa” akatuambia.
Tukamuaga na kutoka. Tukaanza kutembea haraka haraka kwa kufuata ile njia tuliokwendea.
Kisiwa kilikuwa kimya na kilichokuwa kinatisha. Kelele zilizosikika zilikuwa ni za kunguru waliokuwa wakilialia na kurukaruka kwenye miti kama waliokuwa wakiambizana “Hao! Hao! Hao!”
Tulikuwa tukiangalia huku na huku kwa hofu ya kutokewa na Harishi. Kuwa na silaha katika mazingira yale ilikuwa muhimu. Mimi nilikuwa na sime niliyokuwa nimeichomeka kiunoni. Wenzangu wawili walikuwa na mapanga. Wenzetu wengine walikuwa mikono mitupu.
Kwa sababu ya hofu iliyosababishwa na kelele za wale kunguru nilitoa sime yangu na kuishika mkononi. Sasa nikawa tayari kukabiliana na chochote kitakachotokea.
Mpaka tunatokea kule ufukweni mwa bahari tulizungukazunguka sana kwani tulikuwa tunapotea njia mara kwa mara. Kulikuwa na mti mkubwa ulioota kando ya bahari. Tukakaa chini ya ule mti.
Tulitoa vyakula tulivyopewa na Yasmin na kuanza kula. Vilikuwa vhyakula vizuri vikiwa mchanganyiko wa mikate ya mayai, keki, sambusa na biriani.
Wakati tunakula mawazo yangu yalikuwa kwa yule msichana. Kwa kweli nilimuhurumia sana kwa kuishi maisha ya peke yake katika kisiwa kile cha kutisha. Laiti ningekuwa na uwezo wa kumuokoa ningemuokoa lakini ndio hivyo hatukuwa na uwezo na bado sisi wenyewe pia hatukuwa na uhakika wa maisha yetu.
Hata hivyo nilimsifu kwa kuwa na moyo wa kijasiri na wa kiume kwani asingeweza kuishi na kuendelea kuwa hai hadi leo wakati yuko kwenye jinamizi la mauti. Kuishi na jini anayeua watu peke yake lilikuwa ni jinamizi la mauti mbali ya kule kuishi peke yake katika kisiwa kile kinachotisha!.
Nikajiambia kama chombo chetu kingekuwa kizima tungeondoka naye hata kama angekataa.
Baada ya kula kile chakula tulipata akili tukaanza kujadiliana.
“Sasa tufanye nini jamani?” Mwenzetu mmoja akauliza.
“Tuijaribu tena ile boti, inaweza kukubali” nikatoa wazo ambalo lilikubaliwa na wenzangu.
Tukaenda kwenye chombo chetu tukajaribu kukiwasha lakini chombo hakikuwaka. Kila mmoja wetu alijaribu kukiwasha kwa mkono wake. Hakukuwa na yeyote aliyefanikiwa.
Tukaamua kujitia ufundi kuanza kuichokoresha mashine ya boti. Kila mmoja alitia ufundi wake lakini pia hatukufanikiwa. Mimi nilijitupa chini kwenye mchanga nikawaacha wenzangu wakiendelea kushindana nayo.
Yalipita karibu masaa mawili. Hatimaye niliona wenzangu mmoja mmoja akiondoka kwenye boti na kutafuta mahali pa kukaa. Wote walikuwa wamekata tama kama nilivyokata mimi.
Mawazo yangu yakarudi kwa Harishi. Kama alivyotwambia Yasmin Harishi anaweza kutokea na kutumaliza kama alivyowamaliza watu wa kisiwa hicho.
Kwa muda sote tulikuwa kimya. Kila mmoja alikuwa akiwaza lake. Tulipokitokea kisiwa kile tuliona tuliona tumeokoka tukafurahi. Kumbe tumeepuka kufa maji, tumekwenda kwa muuaji mwingine anayefyonza damu.
Tuliendelea kukaa pale tukiangalia baharini hadi jua likaanza kuchwa. Hatukuona chombo chochote kilichopita karibu. Tulichokiona ni mawingu yaliyoonekana kama yanazama upeoni mwa macho yetu.
Wakati giza linaingia hatukujua tungejisitiri mahali gani usiku huo kwani kwa vyovyote vile tusingeweza kuupitisha usiku mahali hapo kutokana na baridi. Pia usalama wetu ulikuwa mdogo. Lolote lingeweza kutokea wakati wa usiku. Kuna vitu kama majoka na wanyama wakali ambao hujificha wakati wa mchana na kujitokeza wakati wa usiku.
Baada ya kuufikiria usalama wetu tulishauriana turudi tena katika lile jumba la yule msichana. Kuna waliopinga wakataka tupande juu ya mti ule tuupitishe usiku.
Lakini upepo mkali ulioanza kuvuma pamoja na ngurumo za radi ndio uliofanya tukubaliane kwa pamoja kurudi katika lile jumba kwani tulijua muda si mrefu mvua kali ingenyesha na kututosa.
ITAENDELEA

SEHEMU YA 06

Si tu tuliona tungeweza kujisitiri katika lile jumba pia tungeweza kufanya uchunguzi wetu na kujua kama huyo Harishi tuliyeambiwa ameshakuja au bado.
Tukaanza tena safari ya kurudi katika lile jumba. Mvua ilikuwa imeshaanza kunyesha kidogo dogo huku upepo mkali ukiendelea kuvuma pamoja na radi.
Tulitembea kwa mashaka mashaka tukikwepa kuwa karibu na miti kwa kuhofia kupigwa na radi.
Kulikuwa giza na hatukuweza kupata mwanga ila pale radi ilipopiga ndipo tulipoona tulikokuwa tunaelekea. Kutokana na giza hilo tulihangaika katika pori kwa muda kabla ya kufanikiwa kutokea katikati ya ule mji uliohamwa.
Tulikuwa tunaendelea kutota na mvua na huku tukiendelea kwenda. Tukawa tunalitafuta lile jumba. Tulidhani tusingeliona kwa urahisi lakini lilikuwa linawaka taa. Tukaliona kwa mbali. Tukalifuata.
Kwanza tulinyata kwenye madirisha. Tukawa tunachungulia na kutega masikio kusikiliza. Hatukusikia sauti yoyote. Kulikuwa kimya. Ndipo tukaamua tuingie.
SASA ENDELEA
Tukaingia ndani ya jumba hilo lililokuwa linawaka taa ndani. Lakini tuliingia kwa kunyata ili hatua zetu zisisikike. Jumba hilo lilikuwa kimya kama vile tulivyoliacha mchana.
Kila tulipofikia kona tulichungulia kwanza kabla ya kuendelea kwenda. Tukaenda hadi katika kile chumba tulichomkuta Yasmin binti wa rais wa Comoro.
Mlango wa chumba hicho ulikuwa umefungwa. Tukaenda jikoni tukapekua pekua na kukuta vyakula vilivyokuwa vimebaki. Tukakaa chini na kuanza kula kwani njaa ilikuwa inatuuma na hatukutarajia kupata chakula usiku huo.
Baada ya kula tulitoka humo jikoni tukaamua kutafuta mahali pa kulala ndani ya jumba hilo hilo. Karibu vyumba vyote tulivyofungua ukiacha kile cha Yasmin vilikuwa na vitanda. Kila kitanda kilikuwa na chumba kimoja kilichowezesha kulala watu wawili.
Tukaamua tulale kila chumba watu wawili. Tulikuwa tupo saba. Mmoja wetu akaamua kuchukua godoro kutoka chumba kingine na kuliingiza katika chumba tulichokuwemo mimi na mwenzangu. Akalilaza chini. Kwa vile yeye hakuwa na mwenzake wa kulala naye na asingeweza kulala peke yake, ndipo aliamua kuja kulala na sisi.
Mvua likuwa inaendelea kunyesha na radi ilikuwa inapiga. Kama tungekuwa tuko kwenye boti yetu tungejuta.
Mimi nilisoma aya zangu kisha nikajifunika shuka. Naamini na wenzangu kila mmoja alisoma dua yake kabla ya kulala.
Tulikuwa tumepanga tuamke alfajiri tutoke kwenye hilo jumba bila hata kumshitua Yasmin.
Hata hivyo usingizi hatukuupata kirahisi kwa sababu ya hofu. Tuliendelea kukaa macho hadi usiku mwingi. Wenzangu walipata usingizi lakini mimi sikulala.
Kulikuwa na wakati usingizi ulikuwa umeanza kunijia nikaamshwa na mwenzetu aliyekuwa amelala chini.
“Unasemaje?” nikamuuliza.
“Mkojo umenibana nisindikize chooni” akaniambia.
Vyoo vilikuwa nje.
Nikatenga shuka na kunyanyuka. Mwenzangu niliyelala naye alikuwa anakoroma.
“Twende!” nikamwambia yule aliyeniamsha.
Tukatoka pamoja. Vyoo vilikuwa ukumbini karibu na mlango wa kutokea.
Tulikwenda hadi karibu na milango ya vyoo. Kulikuwa na vyoo vinne. Mwenzangu alishaingia choo kimojawapo. Mimi nikasikia hatua za mtu nyuma yangu nikageuka. Alikuwa ni yule mwenzetu tuliyemuacha amelala, naye aliamka na kutufuata.
Alikuwa anakuja harakaharaka kutukimbizia. Nilijua ni sababu ya uoga. Wakati huo huo nikaona mlango wa chumba cha Yasmin unafunguliwa. Nikaingia chooni haraka ili niweze kumchungulia aliyekuwa anatoka bila yeye kuniona.
Ghafla nikaliona jitu likitoka katika kile chumba. Lilikuwa jitu la kutisha lililojifunga kilemba kikubwa. Lilikuwa na msitu wa nywele zilizotokeza nje ya kilemba chake. Lilivaa kanzu nyeupe iliyochafuka kwa madoa ya damu na iliyokatwa mikono.
Mikono yake minene iliyoota manyoya marefu ilikuwa imeshupaa. Mkono mmoja alishika upanga mrefu.
Uso wake ulikuwa na ndevu nyingi na sharafa kiasi kwamba sura yake haikuweza kutambulika. Kilichoonekana kwenye uso wake ni pua yake iliyofura kamailiyopachikwa na macho yake makubwa yenye makengeza.
Miguu yake ilikuwa pekupeku. Alikuwa na vidole virefu na vinene vya miguu, tena vilikuwa na kucha ndefu kama kucha za mnyama.
Hapo hapo nikahisi kwamba yule alikuwa ndiye Harushi. Alikuwa ametufuma vizuri ndani ya hilo jumba.
Uso wake ukiwa na hasira kali, macho yake ya makengeza yalielekea kwa yule mwenzetu aliyekuwa anatufuata. Alikuwa ameshafika karibu yake kiasi kwamba jitu hilo lilinyoosha mkono wake wa kushoto na kumshika shati.
ITAENDELEA

SEHEMU YA 07

“Mimi nasikia harufu ya binaadamu humu ndani. Kumbe ni wewe!” akamwambia yule mwenzetu aliyemshika shati. Suati yake ilikuwa ya kuunguruma kama gari bovu.
Wakati anasema meno yake yalitoka nje. Yalikuwa meno marefu kama ya nyani!
Alipomshika mwenzetu shati alimvuta karibu yake.
“Umeingiaje humu ndani na umefuata nini….kwanza umetoka wapi?” akamuuliza kwa hasira.
Ghafla Yasmin akatoka.
“Ni nani?” akauliza huku akimtazama yule mtu ambaye alikuwa akitetemeka.
Yasmin alipomuona alimgundua.
“Itakuwa ni wavuvi walioharibikiwa na chombo chao, wameona nyumba wameingia wakidhani watapata msaada” Yasmin akaliambia lile jitu.
“Anaingia humu anamfuata nani. Huyu simuachi ng’o!” jitu hilo lilisema na kumshika yule mwenzetu kwenye kiuno kisha likamuinua juu kwa mkono mmoja na kumgeuza kichwa chini. KIchwa cha mwenzetu kikawa chini ya kichwa cha jitu lile jitu.
Ndipo jitu hilo lilipokita utosi wa yule mtu kwa ncha ya upanga wake. Mwenzetu huyo alipiga ukulele mmoja tu “Nakufaaa!” kisha akawa kimya. Damu ikaanza kuchuruzika kutoka kwenye utosi wakei jitu hilo likakinga mdomo wake na kuanza kuifyonza!.
SASA ENDELEA
Aliendelea kuinywa ile damu iliyokuwa ikitoka kama maji ya bomba. Mwisho alibandika mdomo wake pale kwenye utosi na kuanza kufyonza.
Nilikuwa nikitetemeka kwa hofu kama niliyepatwa na homa ya baridi ya ghafla. Nilijua akimalizwa yule mwenzetu itaanza zamu yetu sisi kwani sote tulikuwa ndani ya lile jumba.
Midomo ya Harishi ilitapakaa damu. Damu nyingine ilikuwa inavuja midomoni mwake na kuingia kwenye ndevu zake na kisha kutiririka hadi kwenye kanzu yake.
Yasmin alikuwa ameshika kichwa chake kwa huzuni na alikuwa amekiinamisha kichwa chake chini ili asiangalie lile tukio.
Pamoja na huzuni na uchungu vilivyompata Yasmin bila shaka alikuwa akijiambia “Wameyataka wenyewe. Nilishawambia waondoke, kumbe wamerudi tena”
Nikaona mafunda ya Harish yanafutuka huku akitafuna kwa haraka haraka na kumeza. Kumbe alikuwa alikuwa anafyonza ubongo wa mwenzetu na kuula. Aliula kwa ulafi. Mwingine ulimvuja midomoni na kuingia kwenye ndevu zake.
Alipotosheka alitupa chini ile maiti akaanza kujirambaramba midomo na kujifuta kwa mkono. Alipomaliza aliinama akaushika mguu wa yule mtu aliyemuua.
“Sasa nimeshiba vizuri, ngoja niondoke” alijisemea peke yake akiuinua ule mguun na kuuburuza kuutoa ule mwili nje. Aliuburuza huku akiendelea kujirambaramba. Alipofika kwenye mlango aliufungua na kutoka na ile maiti nje.
Yasmin alikuwa bado amesimama akimtazama.
“Lakini mimi niliwambia ila hawakunisikia” akajisemea peke yake huku akitikisa kichwa.
Kwa sababu ya kuzidiwa na hofu na kujua kuwa sote tutakufa nilijitokeza pale nilipokuwa nimejificha. Nikamfuata Yasmin.
Yasmin alishituka aliponiona.
“Na wewe umetokea wapi?” akaniuliza kwa kutaharuki.
“Nilikuwa nimejificha chooni” nikamjibu kwa sauti ya kutetemeka.
“Unaiona damu hii ya mwenzenu?”
Yasmin akanionesha damu iliyokuwa imedondoka chini.
“Nimeiona na nimeona pia alivyouawa”
“Si niliwambia mwendezenu?”
“Tulirudi huu usiku tulipoona kuna mvua na hatukuwa na mahali pa kujisitiri”
“Sasa mmerudi na Harishi ametokea. Mwenzenu ameonekana”
“Kwani atarudi tena usiku huu?”
“Usiku huu hatarudi tena lakini kama ameshasikia harufu zenu anaweza kurudi hata kesho akijua atapata mlo mwingine. Yule hali kitu isipokuwa damu na ubongo. Watu wa kisiwa chote hiki amewamaliza yeye na ana nguvu zisizo za kawaida. Yule mtu amemuinua juu kwa mkono mmoja tu”
“Na amempeleka wapi?”
“Amekwenda kumtupa nje ili asubuhi aliwe na kunguru”
“Sasa sijui sisi tutakimbilia wapi kwani chombo chetu kimekataa kabisa kuwaka”
“Mimi sina la kuwambia kwani popote mtakapokwenda ndani ya kisiwa hiki atawagundua na atawamaliza mmoja mmoja”
Nilibaki kuduwaa na kutikisa kchwa. Kwa mara ya kwanza niliona kazi ya uvuvi ilikuwa mbaya. Laiti kama ningejua kuwa chombo chetu kingeharibika baharini nisingeshiriki katika safari ile.
“Wenzako wengine wako wapi?” Yasmin akaniuliza.
“Nikwambie ukweli Yasmin, sisi tulirudi mapema huu usiku tukaigia jikoni na kula chakula chako kwa sababu tulikuwa na njaa. Tukaingia vyumbani kulala. Sasa tulitoka watu wawili kuja kujisaidia. Huku nyuma mwenzetu mmoja naye alitoka peke yake, Ndiye yule aliyekamatwa na kuuawa”
“Wenzako wengine wako wapi?”
“Mmoja amejificha chooni na wenzetu wengine wako vyumbani”
“Sasa na nyinyi nendeni mkalale, asubuhi mtafanya maarifa. Yule jini hatarudi kwa leo, ameshashiba”
Yule mwenzangu aliyekuwa chooni aliposikia maneno yale alitoka haraka. Yasmin akamtazama.
“Nyinyi mna bahati sana. Angeweza kushikwa mmojawenu”
“Ni kweli kwa sababu sisi ndio tuliotoka kwanza” nikamwambia Yasmin.
“Basi nendeni mkalale”
Tukarudi kwenye vile vyumba. Yasmin alikuwa bado amesimama akituangalia hadi tulipofungua mlango na kuingia chumbani’
Wala hatukulala kamwe. Mimi nilikaa macho usiku kucha nikimuwaza yule mwenzetu aliyeuawa kikatili.
“Nyinyi mna bahati sana. Angeweza kushikwa mmojawenu…” nikawa nayakumbuka maneno ya Yasmin huku mwili ukinisisimka kwa hofu.
ITAENDELEA

SEHEMU YA 08

Mara kwa mara nilikuwa nikitupa macho kila upande wa chumba hicho kwa hisia kwamba Harishi angeweza kutokea mle chumbani.
Asubuhi kulipokucha Yasmin alikuja kutugongea mlango.
“Amkeni. Kumeshakucha” Alikuwa akituambia wakati akigonga. Tukatambua kuwa alikuwa ni yeye.
Tukafungua mlango.
“Mmeamkaje?” akatuuliza.
“Tunashukuru tumeamka salama” nilimjibu kwa niaba ya wenzangu.
Wenzetu waliolala chumba kingine walikuwa hawana habari ya tukio lililotokea usiku. Nikawaeleza mbele ya Yasmin. Wakasikitika sana na kupata hofu.
“Sasa nendeni mkaoge halafu niwaandalie chai” Yasmin akatuambia.
Tukaenda kuoga. Kwanza waliingia watu wanne kwa vile vyoo vilikuwa vine. Walipotoka nikaingia mimi na mwenzangu.
Yasmin akatuandalia chai pale sebuleni. Ilikuwa chai iliyotengezwa kwa maziwa ya unga na iliyoungwa kwa iliki, tangawizi na bdalasini. Pia alitupa mikate iliyotengezwa kwa mayai.
SASA ENDELEA
Yeye mwenyewe alikunywa chai pamoja na sisi. Nikamuona amefurahi na kuchangamka licha ya kwamba usiku wa jana yake tu tulishuhudia machungu ya kuuawa mwenzetu.
“Ningekuwa nakula na wageni kila siku namna hii ningechangamka, lakini mh!” Yasmin alisema kama aliyekuwa akisema pek yake.
“Ni kweli Yasmin lakini tutafanyaje? Tunapenda kukusaidia lakini hatuna uwezo. Kama hivyo umeona mwenzetu ameshauawa na sisi hatujui maish yetu yatakuwaje!” nikamwambia Yasmin kwa huzuni.
“Kusema ukweli napenda niendelee kuwa na nyinyi hapaili nipate wenzangu wa kuzungumza nao. Lakini haitawezekana nyinyi muwepo hapa mkiwa hai.”
“Na pia hatuna mahali pengine pa kwenda” nikamwambia Yasmin.
“Huu ni mtihani. Sijui mtatumia mbinu gani muwe salama”
“Labda tuendelee kujifichaficha humu ndani” Mwenzetu mmoja akaingilia yale mazungumzo.
“Humu ndani atawagundua tu” Yasmin akamjibu.
“Sasa tutakwenda wapi jamani!”
“Mimi sijui niwambie nini ndugu zangu!” Yasmin akatuambai.
Tulipomaliza kunywa chai Yasmin aliondoa vyombo. Alituacha tumekaa tukiendelea kujadiliana. Baadaye kidogo alirudi akiwa na karata.
“Hizi karata ziko siku zote. Huyu mwendawazimu ananiletea. Lakini sina mwenzangu wa kucheza naye”
Tulipoona karata tukazunguka duara. Yasmin akakaa na kutugawia.
“Tunacheza mchezo gani?” nikamuuliza Yasmin.
“Tunacheza mchezo wa arbasitini”
Mchezo huo ulikywa maarufu kule Zanzibara na Comoro.
Tukaanza kucheza karata. Tukasahau kabisa habari ya Harishi. Mchezo ulinoga sana. Kelele zetu zikawa zinasikika hadi nje.
Ilipofika saa tano Yasmin akavunja mchezo na kutuambia tukatembee tembee. Tukiona jua la saa saba ndio turudi kula chakula. Mda ule alitaka kwenda kupika chakula.
“Niwapikie nini?” akatuuliza.
“Tupikiechochote tu utakachopenda” nikamwambia.
“Basi nitawapikia pilau”
“Tutashukuru sana”
“Sasa mtakapokuja, kwanza mchungulie na kusikiliza. Mkimuona Harishi msiingie ndani, rudini huko huko mtakakotoka. Anaweza kuja ghafla”
“Tumekuelewa” nilimjibu.
Baada ya hapo tulitoka tukarudi kule kwenye boti letu.
Ni tabia ya maumbile ya binaadamu kutokata tama na kujaribu kubahatisha kila mara hasa kwa watu kama sisi ambao tulikuwa katika hatari. Kwa mara nyingine tulijaribu tena kuliwasha lile boti. Kila mmoja wetu alijaribu kuliwasha bila mafanikio.
Tukakaa chini ya mti na kuanza kujadiliana. Hata hivyo mjadala wetu ulikuwa kama usio na maana yoyote kwani haukutupa ufumbuzi wa jinsi ya kusalimisha maisha yetu.
Kikubwa tulichokizingatia ni kujaribu kumkwepa Harish kadiri itakavyowezekana. Tuliona kama tutafanikiwa kumkwepa tunaweza kuendelea kuishi.
Tuliendelea kukaa pale chini ya mti hadi saa saba tulipoamua kurudi kwa Yasmin. Tulimtuma mmoja wetu aingie akachunguze kama Harishi yuko ndani aje atuambie.
Mwenzetu huyo akaingia ndani. Sisi tukawa tunamchungulia kwenye dirisha. Alinyata hadi ndani. Tukawa hatumuoni tena. Tukahamia kwenye dirisha jingine. Tukamuona amesimama pembeni mwa ukumbi akiangalia huku na huku. Akaenda jikoni kuchungulia kisha akatoka.
Alipotoka jikoni alikwenda moja kwa moja kwenye mlango wa chumba cha Yasmin na kutega masikio yake kwenye mlango. Alisikiliza kwa muda kidogo kisha akaanza kugonga mlango taratibu.
Mlango ukafunguliwa ghafla. Aliyetoka alikuwa Yasmin. Alitoka haraka haraka akaufunga mlango kisha akamuashiria yule jamaa aondoke. Nikajua kuwa hapakuwa salama.
“Moshi unajaa kwenye chupa, Harishi anakuja!” Yasmin alimwambia.
Yule mwenzetu aliposikia vile aligeuka ili aondoke lakini ghafla tena mlango ukafunguliwa. Harish akaibuka mbele ya yule mtu. Alikuwa ameshika upanga wake. Akamshika yule jamaa kwa mkono mmoja.
“Unataka ukimbie wapi wewe?” akamuuliza akiwa amemtolea macho.
ITAENDELEA

SEHEMU YA 09

Mwenzetu aliishiwa na nguvu kabisa. Akawa amemkodolea macho Harishi.
“Mimi nasikia harufu zenu tangu jana”
Mwenzetu kimya. Sasa mwili wake ulikuwa ukitetemeka waziwazi.
“Sheikh nisamehe sana…” Sauti yake ikasikika kwa mbali ikiomba.
“Chombo chetu kiliharibika jana”
Harisha alikuwa akimtazama kama vile alikuwa hamuelewi.
“Wasemaje?”
“Nisamehe sana…nakuomba” jamaa alikuwa analia.
“Kwani wewe huna damu?. Ngoja nione”
Hapo hapo Harishi akamuinua juu mwenzetu huyo kwa mkono mmoja tu. Akamgeuza kichwa chini.
Kiasi cha kufumba na kufumbua tu alishamtoboa utosi kwa ncha ya upanga wake.
Yasmin alipoona hivyo alikimbilia nje. Akatuona tumeinamia dirisha.
“Jamani balaa gani hili?” akajisemea peke yake.
SASA ENDELEA
Idadi yetu sasa tulikuwa watu watano, wenzetu wawili walikuwa wameshauawa. Na sisi pia hatukuwa na matumaini kuwa tungebaki.
Tulijua kuwa kama hatutakufa kwa njaa, tutauliwa na lile jini la Yasmin. Kila mmoja wetu alikuwa ameshikwa na hofu na fadhaa. Tulitamani angalau kipite chombo kituokoe kuliko vile tulivyokuwa matumatu tukisubiri kufa.
Tulitamani tusifike tena katika lile jumba la Yasmin lakini tungekula nini, wakati kwa Yasmin ndiko tunakotarajia kupata riziki yetu. Kusema kweli tulichanganyikiwa na hatukujua la kufanya.
Tulikaa pale chini ya mti kwa karibu saa mbili. Ghafla tuliona mwanamke akiambaa na ufukwe wa bahari akija upande wetu. Mkono mmoja alikuwa ameshika kapu.
“Jamani ni nani yule?” Mwenzetu mmoja akauliza.
“Naona ni kama Yasmin” nikajibu.
Mjadala ukaanza.
“Ni Yasmin kweli!”
“Amefuata nini huku?”
“Labda anatutafuta sisi”
“Mmoja wetu atokeze ili atuone au aende akampokee lile kapu. Labda anatuletea chakula”
“Hatujui Harishi yuko wapi. Unaweza kujitokeza ukajikuta unakamatwa!”
“Bila shaka Harishi ameshaondoka, Yasmin asingeweza kuja huku. Ngoja nimfuate” Mimi ndiye niliyesema hivyo. Nikanyanyuka na kuanza mwendo kuelekea upande ule aliotokea Yasmin.
Yasmin akaniona.
“Nawatafuta nyinyi, mko wapi?” akaniuliza tangu akiwa mbali.
“Tuko huku chini ya mti. Tumekuona tangu ukiwa mbali”
“Nimewaletea chakula”
Nilikuwa nimeshamfikia. Nikampokea lile kapu.
Tukawa tunatembea pamoja kuelekea kule waliko wenzetu
“Lile shetani limeshaondoka, ndio maana nimeweza kutoka” Yasmin akaniambia’
“Halitarudi tena kwa leo?”
“Halitarudi labda kwa kesho”
“Yule mwenzetu ndio ameuawa?”
“Ndio aliuawa. Si mliona wenyewe akikamatwa”
Nikatikisa kichwa changu kusikitika.
“Wakati anabisha mlango niliona ile chupa ya Harishi inajaa moshi. Nikajua kuwa Harishi anakuja. Nikawahi kutoka ili niwambie muondoke. Wakati nasemeshana na yule mwenzenu, Harishi akasikia akawahi kutoka na kumkamata” Yasmin aliendelea kunieleza.
“Sasa yule jinni atatumaliza sote. Tulikuwa watu saba sasa tumebaki watano tu”
“Basi msije kule”
“Sasa tusipokuja utatuletea chakula?”
“Nitawaletea. Na leo ameshakula mtu mmoja harudi tena hadi kesho”
Tukawa tumefika walipokuwa wenzetu.
“Leo tumepata msiba mwingine” Mtu mooja akamwambia Yasmin.
“Nilishawambia tangu mapema kuwa usalama hapa ni mdogo sana kwa sababu ya Harishi. Sasa mnaona wenyewe, na ijui mtafanya nini ndugu zangu”
“Jamani kwanza tuleni chakula. Yasmin ametuletea chakula. Tukanawe mikono kwa maji ya chumvi. Mazungumzo baadaye” nikawambia wenzangu.
Tukaenda kunawa maji ya bahari kisha tukarudi pale chini ya mti, tukaketi. Yasmin naye akaketi.na sisi. Tukaanza kula.
“Kwani Harish ameshaenda zake?” Mtu mmoja akamuuliza Yasmin.
“Ameshaondoka” nikamjibu mimi. “Angekuwepo Yasmin asingeweza kuja huku”
Fuatiliakisahiki hapo na usikose
ITAENDELEA

SEHEMU YA 10

Tulikula pilau ikiwa ndani ya kapu. Tukashiba na kupata nguvu.
“Nimesahau kuwachukulia maji ya kunywa” Yasmin akatuambia.
“Na maji tuliyokuwa nayo yamekwisha” nikasema.
“Lakini kwa leo Harishi hatarudi, mnaweza kuja nyumbani” Yasmin akatuambia.
“Mh!. Nyumbani kwako kunaogopesha” nikamwambia Yasmin.
“Tunaweza kwenda mnywe maji halafu mtarudi huku huku”
Tukajadiliana na Yasmin, mwisho tukaamua turudi katika lile jumba. Tukarudi.
Tulipofika alitupatia maji ya kunywa. Tukamshukuru kwa wema wake.
“Bado mna wasiwasi?” Yasmin akatuuliza.
“Kuwa na wasiwasi ni lazima” nikamjibu na kuongeza. “Tunajiona kama tuko kwenye vita”
“ Kwa leo msiwe na wasiwasi. Yule jini hatarudi tena. Kama ni kurudi ni kesho. Tunaweza kukaa tukaongea hadi usiku mkaenda zenu”
Tukashauriana na kukubaliana tukae hadi usiku kwa vile mwenyeji wetu ameshatuhakikishia kuwa tutakuwa salama. Pia tulikuwa tunamuhurumia Yasmin aliyekuwa mpweke katika jumba lile. Tukaona tukae tumchangamshe.
Tukakaa kwenye ule ukumbi pamoja na Yasmin na kuanza kuzungumza.
“Yasmin alitupa hadithi ya jinsi alivyofikishwa katika jumba lile na jinsi alivyokuwa akilia katika siku za mwanzo mwanzo.
ITAENDELEA
.
“Lile jini hata ukilia, halijali. Linakwambia utazoea tu. Na ni kweli kadiri siku zilivyokwenda nilijikuta nikizoea” Yasmin aliendelea kutuhadithia.
“Sasa mnaishije, wakati wewe ni mtu na yule ni jini?” Mwenzetu mmoja akamuuliza.
“Tunaishi kama mke na mume ingawa mwenzangu ni jini lakini ndio nimeshamzoea. Ameshaniambia kwamba nitaishi naye hadi kufa kwangu”
“Je kama akifa yeye?” nikamuuliza.
“Amesema yeye hatakufa haraka. Umri wa majini ni mrefu sana. Pale alipo ana miaka mia tatu na anaweza kuishi hadi miaka mia tano”
“Loh!. Wewe utakufa, yeye ataendelea kuishi kwa miaka mingi sana” Mtu mmoja akamwambia Yasmin.
“Lakini mimi ningependa kujua hisia zako. Unajisikiaje unapohisi kuwa utaishi ndani a jumba hili hadi ufe wakati bado ni msichana mdogo” Mimi nilimuuliza Yasmin swali hilo.
Yasmin akabetua mabega.
“Nasikia vibaya lakini nitafanyaje sasa. Nimelia nimechoka, sasa silii tena”
“Kwa hiyo ndio unaishi ukisubiri kifo chako kitokee humu humu ndani?” Mtu mwingine alimuuliza. Lilikuwa si swali zuri. Sikulipenda. Lakini Yasmin alimjibu.
“Wakati mwingine najidanganya kwamba iko siku yaweza kutokea miujiza nikaokolewa kwa namna nisiyoijua.
“Na tangu uishi humu hakujatokea watu kama sisi wakaingia katika jumba hili?” nikamuuliza.
“Nyinyi ndio watu wa kwanza kuwaona tangu nianze kuishi katika jumba hili”
Tukaendelea kuzungumza na Yasmin hadi alipotuambia kuwa anakwenda kupika chakula cha usiku.
Tukabaki sisi peke yetu na kuendelea kuzungumza na kujadiliana kuhusu maisha ya Yasmin na maisha yetu wenyewe.
Jua lilipokuwa limekuchwa nilimfuata Yasmin jikoni nikamwambia kwamba tunaondoka.
“Kwanini…subirini mle chakula. Nimepika chakula kingi kwa ajili yenu” Yasmin akaniambia
“Giza linaingia. Tuna hofu yule jini anaweza kutokea. Acha tuondoke tu”
“Jamani mkiwepo mnanichangamsha na mimi. Sasa mnataka kwenda wapi?”
“Tunarudi kule kule ulikotukuta”
“Kwanini jamani? Nimewambia Harishi hawezi kurudi leo labda kwa kesho. Mnaweza hata kulala hapa na mkawa salama. Muhimu ni kuamka kabla hakujapambazuka mwende zenu”
“Unajua tuna hofu na wasiwasi, wenzetu wawili wameshauawa humu humu ndani”
“Sasa kule mtakaaje usiku huu na baridi? Je mvua ikinyesha usiku huu mtafanyaje. Si bora mlale hapa hapa”
“Ngoja nikawashauri wenzangu” nikamwambia Yasmin na kurudi kule ukumbini. Yasmin naye akanifuata.
“Yasmin amesema tusubiri chakula na pia tunaweza kulala hapa hapa” nikawambia wenzangu.
“Tulale hapa hapa?” Mtu mmoja akaniuliza kwa mshituko.
“Hakuna neno. Mnaweza kulala tu ilimradi muamke alfajiri kabla ya kupambazuka mwende zenu” Yasmin akawambia.
“Una hakika kwamba Harish hatakuja usiku huu?’
“Hatakuja tena kwa leo ila kesho anaweza kuja. Sasa kwa vile sijui atakuja saa ngapi ndio maana nninawambia muondoke alfajiri”
Yasmin alipoona wenzangu wameduwaa wakitazamana kutafakari yale maneno yake akatuambia.
“Jamani kuweni na mimi. Hivi nashukuru kupata wenzangu wa kunichangamsha. Harish hatakuja tena leo”
“Mimi naona tumsikilize mwenyeji wetu, acha tukae” Nikawambia wenzangu kwa kumuonea huruma Yasmin.
Pia huko tulikotaka kwenda hakukuwa salama. Tungeweza kushambuliwa na wanyama usiku ule au kunyeshewa na mvua.
Tukakubaliana kuwa tubaki na Yasmin.
“Hakuna lolote litakalotokea, kaeni kwa roho moja. Mimi ndiye ninayejua kawaida na nyendo za Harishi. Mnachotakiwa ni kujihimu wakati wa alfajiri muondoke humu ndani ili kama kesho atatokea asiwakute” Yasmin akatusisitizia kabla ya kurudi jikoni.
Baada ya muda kidogo alituletea chakula, tukala pamoja na yeye.
Tulipomaliza kula Yasmin aliondoa vyombo. Aliporudi tena alikuwa ameshika karata. Akaketi na kutuambia. “Sasa tuchezeni karata, tukichoka tunakwenda kulala”
ITAENDELEA

SEHEMU YA 11

Akagawa karata, tukacheza hadi usiku mwingi. Wenzangu wengine walikuwa wameshaanza kusinzia. Tukavunja mchezo na kwenda kulala.
Tuliingia katika vyumba viwili. Chumba kimoja waliingia watu wawili na chumba kingine waliingia watu watatu. Mmoja aliweka godoro chini. Mimi nilikuwemo katika kile chumba walichongia watu watatu. Nililala kitandani. Na mwenzetu mmoja ndio alilala chini.
Licha ya Yasmin kututoa wasiwasi kuwa Harishi hatatokea usiku ule, hatukulala kwa raha. Mara kwa mara nilikabiliwa na hofu. Nilipolala kidogo nilijikuta ninagutuka na kutupa macho huku na huku.
Wakati inakaribia kuwa alfajiri ndipo nilipopata usingizi wa uhakika. Nikalala moja kwa moja. Sikuzinduka mpaka kumekucha. Kilichonizindua ni hisia zangu. Niliona kama mlango wa mle chumbani unafunguliwa na mtu aliyekuwa nje.
Nilipofumbua macho niliona kweli mlango unafunguliwa na kulikuwa kumeshakucha ingawa Yasmin alituambia tuamke alfajiri na kuondoka.
Nikajiuliza ni nani anayefungua mlango. Nikaona kanzu yenye madoa ya damu ikiingia ndani.
Alikuwa harishi!
SASA ENDELEA
Nilishituka sana nilipogundua kuwa aliyefungua ule mlango alikuwa ni jini Harishi. Tulipaswa kujilaumu kwa uzembe wetu wa kulala hadi muda ule wakati Yasmin alituambia tuondoke kabla hakujapambazuka.
Na kwa kweli haukuwa uzembe bali tulipitiwa na usingizi, tena wakati mimi nazinduka wenzangu wote walikuwa bado wamelala.
Harishi aliingia ndani ya kile chumba. Sasa niliweza kuuona vizuri uso wake. Alikuwa na macho makubwa yenye makengeza.
Nikajifanya kama nimelala lakini nilikuwa nikimuangalia kwa pembeni na kwa makengeza huku mwili wangu ukitetemeka kwa hofu.
Pengine ni kutokana na ale makengeza yake, Harishi alipoingia mle chumbani macho yake yalikwenda kwa yule mtu aliyelala chini.
Mara moja aliinama na kumshika shingo yake kisha akamuinua na kutoka naye ukumbini.
Nikaisikia sauti ya Harishi akiuliza.
“Hii nyumba ni yako?”
Sikusikia jibu bali nilimsikia mwenzetu akipiga ukulele mmoj tu.
“Jamani nakufa!”
Halafu sikusikia kitu tena.
Hapo nilijua mwenzetu huyo alikuwa ameshatoolewa utosi na alikuwa akifyonzwa damu.
Ule ukulele aliopiga ulimuamsha mwenzangu niliyelala naye. Akainuka na kuketi kitandani.
“Kitu gani?” akaniuliza.
Nikaweka kidole changu cha shahada kwenye midomo yangu kumkataza asitoe sauti.
“Nini kwani?” Sasa sauti yake ilikuwa ya chini. Uso wake ulikuwa umeanza kushituka.
Nilishuka kitandani nikamnong’oneza “Harishi!”
Akagutuka. Uso wake ukabadilika na kuvamiwa na hofu.
“Yuko wapi?” akauliza kipumbavu
Sikumjibu. Nikamwambia “Tuingie mvunguni mwa kitanda”
Akakurupuka na kujiingiza kwenye mvungu huku akiburuza shuka aliyokuwa amejifinika. Tulipoingia kwenye mvungu huo tukanyamaza kimya.
Tuliamua kujificha humo japokuwa hatukuwa na uhakika kuwa tutapona. Bada ya muda kidogo tuliona mlango unafunguliwa tena.
Nilimuona mwenzangu anatikisa kichwa kwa hofu. Tuliona miguu ya Harishi ikiingia. Ilikuwa miguu mikubwa iliyochafuka na yenye vidole vyenye kucha ndefu. Ilikuwa pekupeku.
“Kumbe alikuwa ni yule peke yake!” Tukamsikia akisema Peke yake.
Ile shuka ya mwenzangu aliyokuwa akiiburuza ilitokeza nje ya mvungu wa kitanda. Harishi akaiona!
Tukaona mkono wake ukishika ncha ya shuka na kuivuta. Jamaa akaiachia. Shuka yote ikavutwa na kuchukuliwa na Harishi.
“Hizi ni shuka zangu ninazoziiba kwa Wahindi. Imewekwa na nani huku mvunguni?’ akajiuliza mwenyewe kisha akaitupa chini.
Tukaona miguu inageuka na kutoka. Alipotoka tulishukuru. Mimi nilitambaa hadi kwenye mlango, nikaufungua na kumchungulia.
Nilimuona akiinama na kuushika mguu wa mwenzetu aliyemuua, akamburuza kuelekea kwenye mlango wa kutokea.
Mwenzangu alikuwa amebaki mvunguni akinitazama. Nikaufunga mlango taratibu kisha nikarudi mle mvunguni.
“Mwenzetu ameuawa” nikamwambia mwenzangu. “Harishi amemburuza na kutoka naye”
“Alimuona wapi?”
“Mara ya kwanza aliingia ndani, wewe ulikuwa umelala, Akamsomba pale kwenye godoro na kutoka naye kwenda kumuua. Ndio pale ulipoamka”
“Kumbe Yasmin alitaka tufe alipotuambia tulalae humu?”
“Ni makosa yetu sisi. Yasmin alituambia tutoke Alfajiri, sisi tumelala hadi saa hizi kumekucha”
“Lakini ni kweli”
Wakati tunazungumza kwenye mvungu, Yasmin akaingia.
Tulipoona miguu yake tulitoka mvunguni.
“Jamani niliwambia nini?” akatuuliza kwa kutaharuki.
ITAENDELEA

SEHEMU YA 12

Hakukuwa na aliyemjibu. Sote tulikuwa tumeshikwa na fadhaa.
“Si niliwambia mtoke alfajiri, mmelala hadi saa hizi wakati niliwambia kuwa Harishi atakuja leo”
“Ni kweli ulituambia” nikamkubalia.
“Sasa mbona hamkutoka alfajiri?’
“Tumepitiwa”
“Mtanilaumumimi bure jamani!”
Hatutakulaumu hata kidogo. Umetufanyia wema sana”
“Harishi alikuja mapema sana akaniambia anasikia harufu ya kimtumtu. Nikamwambia mtu ni mimi. Akaniambia hebu ngoja. Akatoka kuja kuwatafuta”
“Siku hizi atakuwa anakuja kila siku kwa sababu ameona anapata mlo anaoutaka. Ni lazima mjihadhari”
“Mimi naona tuondoke tu humu ndani” Mwenzangu akasema kwa woga.
“Lakini amekwishakwenda zake. Kwa leo hatarudi tena” Yasmin akatuambia.
“Itabidi tuondoke tu” Mwenzangu alizidi kusisitiza.
“Kwani wenzenu wengine wako wapi?”
ITAENDELEA
“Bado wamelala hadi sasa?” Yasmin akauliza kwa mshangao.
“Naona bado wamelala” nikamjibu.
“Kumbe nyinyi hamuwezi kuamka alfajiri?”
“Tatizo ni kuwa usingizi wenyewe unakuja wakati wa alfajiri” nikamwambia Yasmin.
“Basi ni balaa. Sasa itabidi usiku mwende mkalale sehemu nyingine, mjaribu bahati yenu”
“Tutafanya hivyo”
“Kuna nyumba nyingi hazina watu. Mnaweza kutafuta nyumba nzuri yenye vitanda mfanye makazi yenu. Hapamtakuwa mnakuja mchana tu, muda ambao nitawambia mimi”
“Tumekue;lewa, ngoja niwaamshe hawa mabwana”
Tukatoka pamoja mle chumbani. Tulipotoka tukawaona wenzetu nao wametoka.
“Hivi ndio mnaamka jamani?” Yasmin akawauliza.
“Dadayetu si unajua usingizi hautabiriki?” Mtu mmoja akamjibu.
“Hamkumbuki jana niliwambiaje? Si niliwambia muamke alfajiri muondoke?” Yasmin akawauliza.
“Ni kweli ulituambia lakini ndio tumepitiwa”
“Shakiri ameuliwa leo na Harishi!” nikawambia.
“Unasema kweli?” wakaniuliza kwa pamoja kwa mshituko.
“Ni kwa sababu ya kuchelewa kuamka. Sisis tumeponea chupuchupu baada ya kuingia mvunguni mwa kitanda”
“Basi utakwisha!”
“Yasmin ametupa wazo. Badala ya kulala hapa tutafute nyumba nyingine tuweke makazi yetu. Hapa tutakuwa tunakuja kula chakula mchana katika muda atakaotuambia Yasmin”
“Hivyo itakuwa vizuri” Mmoja wa wenzetu hao akasema.
“Sasa mjitayarishe, ninaenda kuwaandalia chai” Yasmin akatuambia.
Wakati Yasmin anakwenda jikoni, wenzetu wawili waliokuwa wamelala chumba cha pili ilivyokuwa hadi mwenzetu akauliwa.Tukawaeleza.
Kwa kweli walipata hofu.
“Sasa tukishakunywa chai tutoke tukatafute hiyo nyumba” nikawambia wenzangu.
Ilipofika saa nne tayari tulikuwa tumeoga na kunywa chai. Tukamwambia Yasmin tunataka kwenda kutafuta nyumba ya kukaa kwa maana tayari tulishakuwa wakazi wa kisiwa kile na hatukuwa na mategemeo ya kuondoka.
“Kwani mpaka mwende nyote”Yasmin akaniuliza.
“Unataka twende wangapi?” nikamuuliza.
“Mnaweza kwenda wawili, wawili mkabaki”
Mimi na wenzangu tukatazamana lakini sote tulionekana kutoliafikiwazo la Yasmin.
“Acha tu twende sote” nikamwambia Yasmin.
“Basi ngoja niwasindikize, msiniache peke yangu”
“Tukizunguka na wewe itakuwa vizuri” nikamwambia.
“Kwanini?’
“Kwa sababu wewe ndiye mwenyeji wetu, utaweza kutuongoza vizuri”
“Haya basi twendeni”
Tukatoka na Yasmin. Yasmin alikuwa akikijua vyema kisiwa hicho. Alituzungusha mitaa mbalimbali tukiangalia nyumba. Mwisho alitupeleka katiaka nyumba moja ambayo alituambia ilikuwa ya mtu mmoja tajiri wa kisiwa kile.ambaye naye naye aliuawa na Harishi.
Ilikuwa nyumba nzuri lakini ilikuwa imechakaa kwa vile ilikuwa haiishi watu. Tulipoingia ndani tulikuta mavumbi yalikuwa yameenea nyumba nzima.
Tukaanza kazi ya kuisafisha nyumba. Yasmin alitusaidia kufanya usafi. Ilikuwa kazi iliyotuchukua saa kadhaa.
Tulipomaliza tulichota maji kwenye kisima tukaoga kisha tukapumzika. Hapo ndipo tulipoanza kugawana vymba
Nyumba yenyewe ilikuwa ya vyumba vine na sisi wenyewe tulikuwa wanne. Kila mmoja alijichagulia chumba chake alichokipenda. Tulifungua makabati tukatoa mashuka na kutandika vitanda tulivyovikuta humo ndani.
Wakati ninatandika kitanda Yasmin aliniambia nimpe shuka atandike yeye. Nikampa.
“Natamani sana ningekuwa hapa pamoja na nyinyi” Yasmin akaniambia wakati anatandika.
“Ukiwa hapa utatuponzea sote”
“Ninasema tu lakini najua haitawezekana. Unajua katika nyinyi nyote nimekupenda wewe zaidi. Ninatamani ungekuwa mume wangu”
“Hata mimi natamani ungekuwa mke wangu lakini ndio tupo jela. Uhai wetu unahisabika”
“Ni kweli. Usikumbushiie hayo. Tuswali tuombe nusura itufikie”
“Wewe unaswali?” nikamuuliza Yasmin.
“Ninaswali lakini kwa siri sana. Harishi hataki niswali. Swala ndiyo inayonipa matumaini ya kuishi”
“Umenikumbusha jambo zuri sana na sisi tutaanza kuswali”
“Kila mara ninaota kunamtu atakuja kumuangamiza Harish na mtu huyo atakuwa mume wangu”
ITAENDELEA

SEHEMU YA 13

“Unahakika kuwa nitakuwa salama?”
“Harishi hatakuja leo. Ameshakuja asubuhi ni mpaka kesho”
“Ngoja niwaage wenzangu”
Tukatoka ukumbini. Wenzangu walikuwa wameketi wakizungumza. Nikawambia kwa namsindikiza Yasmin.
“Ninakwenda kupika, nitampa chakula awaletee” Yasmin akawambia.
“Yaani utasubiri chakula huko huko?” Mmoja akaniuliza lakini uso wake haukuonesha furaha.
“Ndio atakisubiri” Yasmin akamjibu.
Masudi akawatazama wenzake kabla ya kuniambia.
“Sawa. Sisi tutasubiri”
Jina lake lilikuwa Masudi. Katika sisi watu wanne tuliobaki, yeye alikuwa ndiye mkubwa kwetu kiumri.
SASA ENDELEA
Wakati mimi na Yasmin tunatoka kwenye ile nyumba tukirudi nyumbani kwa Yasmin, Yasmin aliniambia. “Yule kaka uliyezungumza naye anaitwa nani?’
“Anaitwa Masudi”
“Naona kama hakufurahi ulivyomwambia tunatoka mimi na wewe”
“Inawezekana, ni binaadamu. Labda ameona tumewabagua”
“Mbona wengine hawakusema kitu?”
“Kila mtu ana mawazo yake. Yule amezoea kutuamrisha kwa sababu kwenye kundi letu yeye ndiye mkubwa kiumri na amekuwa kama kiongozi wetu”
“Kwa hiyo alitaka anisindikize yeye”
Yasmin aliposema hivyo nilicheka, na yeye akacheka.
“Unafikiri nakutania?” aliponiuliza hivyo alitaja jina langu.
“Hunitanii, unaniambia ukweli. Najua Masudi hakufurahi” nikamwambia.
Pakapita kimya kifupi kabla ya Yasmin kuniambia.
“Kisiwa chote hilki kilikuwa kina watu”
“Wewe uliwakuta hao watu?” nikamuuliza.
“Wakati Harishi ananileta hapa alikuwa ameshamaliza watu wote. Wengine walihama wenyewe kukimbia kifo”
“Na kama leo anakuja na kutukuta hivi itakuwaje?”
“Atakukamata wewe. Atakufyonza damu na ndio ataniuliza wewe ni nani na ulifuata nini hapa”
“Ina maana wewe hatakuadhibu?”
“Ananitisha tu pale ninapomuudhi lakini kama atanikuta na mwanaume nadhani ataniadhibu”
“Lakini hatakufyonza damu?”
“Hapo siwezi kujua”
“Inatisha. Ni kwa vile tu umenihakikishia kwamba hatarudi tena leo”
Tulipofika katika jumba la Yasmin. Tulikaa katika ule ukumbi tukaanza kuzungumza.
Yasmin akanieleza wazi kuwa alikuwa amenipenda.
“Wewe ndio ungefaa uwe mume wangu” akaniambia kiudhati.
“Tayari umeshakuwa mke wa jini, huwezi tena kuwa mke wangu”
“Jini amenioa wapi? Si ananibaka tu!”
“Lakini ndio mume wako na amekuleta huku kusudi aweze kukudhibiti”
“Hakuna kisichokuwa na mwisho. Mwisho wake utafika tu”
“Inshaallah!”
“Mimi na wewe tutakwenda kuoana Comoro!”
Nikatikisa kichwa changu. Niliona Yasmin alikuwa anaota ndoto ya mchana.
“Yasmin huoni kuwa tuko jela! Unawazia kwenda kuoana Comoro, hapa tutatoka vipi?”
“Tutatoka tu iko siku. Kila siku mimi naswali kuomba”
“Angekuwa ni mwanaadamu aliyekuweka hapa tungepambana naye. Lakini jini aliyemaliza kisiwa kizima ni hatari”
“Usikate tama, usinivunje moyo. Wewe mwanaume!” Yasmin aliposema hivyo alinyanyuka.
“Ngoja nikapike sasa” akaniambia na kuelekea jikoni.
Wakati anatembea nilimtazama kwa nyuma. Nguo alizokuwa amevaa zilimpendeza. Kama alivyotueleza mwenyewe nguo hizo alikuwa naletewa na Harishi ambaye huziiba kwnye maduka ya miji mikuwa.
Yasmin alipofika kwenye mlango wa kuingilia ndani aligeuka na kunitazama. Alipoona nilikuwa namuangalia akatabasamu kabla ya kuingia ndani.
Nilikaa peke yangu nikiwaza hili na lile. Nilijiambia Yasmin alikuwa msichana mzuri, kikwazo kilikuwa ni lile jini. Kama nafanikiwa kumuoa binti wa rais ni heshima kubwa.
Baada ya muda kidogo niliondoka nikamfuata Yasmin jikoni.
“Umenifuata huku?” Yasmin akaniambia.
“Nataka tusaidiane kupika” nikamwambia kwa mzaha.
“Si ungekaa tu nikakupikia mume wangu mtarajiwa”
Nilijua Yasmin alikuwa anajifariji kuniita “mume wangu mtarajiwa” Na mimi sikutaka kumvunja moyo. Kwa upande mwingine mimi pia nilihitaji faraja kutoka kwa Yasmin.
“Hapana nataka nikusaidie mtarajiwa wangu”
“Haya nisaidie”
Nikamsaidia Yasmin kupika huku mizaha na dhihaka zikipita. Kwa mara ya kwanza niligundua Yasmin alikuwa mchangamfu na aliyependa mzaha. Alikuwa akicheka hadi sauti yake ilisikika nje. Alikuwa amesahau kabisa mateso yaliyokuwa yanatukabili sisina yeye.
“Yasmin unacheka sana, sauti yako inasikika nje” nikamwambia.
“Kwani nani atatusikia, si tuko peke yetu?”
“Najua tukompeke yetu lakini usicheke sana”
ITAENDELEA

SEHEMU YA 14

“Acha nifurahishe moyo wangu nisife na kinyongo”
“Sikuwa nikijua kuwa umchangamfu kiasi hicho”
“Mimi ni mchangamfu sana, sema hili jinni ndilo limeniharibia maisha yangu. Ningeweza kuliua ningeliua”
“Hata ukiliua utaondoka vipi hapa kisiwani?”
“Hayo yatakuwa masuala mengine, bora nimeshaliua”
“Kama boti yetu ingekuwa nzima tungekutorosha tukaenda Zanzibar”
“Halafu ungenioa huko huko”
“Upendavyo”
“Mimi ningependa unioe Zanzibar. Gharama zote angetoa baba yangu”
“Mimi nisingekuwa na amri zaidi ya kukusikiliza wewe”
Nilipomwambia hivyo Yasmin alifurahi sana. Chakula kilipokuwa tayari alikipekua sehemu mbili. Sehemu moja ilikuwa yetu mimi nay eye. Sehemu ya pili ilikuwa ya wenzetu.
“Sasa wapelekee halafu urudi tuje tule” Yasmin akaniambia.
Alinitilia chakula kwenye kapu nikaondoka. Wakati nakaribia kufka kwenye mlango wa kutokea, nikawaona wenzangu wamenifuata.
“Tumeona unachelewa, tukapata wasiwasi” Masudi akaniambia.
SASA ENDELEA
“Nilikuwa nasubiri chakula na ndicho hiki ninawaletea” nikamwambia Masudi.
“Sasa na sisi tumeshakuja. Kuna haja ya kwenda tena kule”
“Tunaweza kula hapa hapa”
Masudi akawatazama wenzake.
“Jamani tuleni hapa hapa, au mnasemaje?’ akawauliza.
“Popote tu tunaweza kula”
Nikarudi ndani na kuliweka lile kapu la chakula.
Yasmin alikuwa amesikia sauti zetu akatufuata.
“Jamani mmekuja huku huku?” akawauliza.
“Tuliona mwenzetu anachelewa tukapata wasiwasi. Tulidhani labda ameshikwa na Harishi” Masudi akamjibu.
“Hapana. Alikuwa anasubiri chakula, lakini mnaweza kula hapa hapa”
Yasmin akaandaa kile chakula kwenye mswala. Kwa vile wenzetu walikuwa wamekuja, tuliona tule pamoja. Yasmin akaleta na kile chakula kingine.
Tulipomaliza kula tuliendelea kuzungumza pale pale tukiwa pamoja na Yasmin.
Masudi alikuwa akimtania sana Yasmin huku akimsifia kwa uzuri. Yasmin alikuwa akichekacheka tu na kuficha uso wake uliokuwa umejaa aibu.
Masudi akaeleza kisa ambacho nilihisi kilikuwa cha uongo kwamba zamani alipokuwa anakaa Mombasa alipendana na msichana mmoja wa Kilamu.
“Msichana. Alikuwa mzuri huyo. Alinipenda na mimi nilimpenda lakini wanawake wa Mombasa hawaoleki bwana!”
“Kwanini?” nikamuuliza.
Wana gharama sana. Huyo msichana wangu alikuwa anaitwa Nargisi. Kila siku alikuwa amechorwa piku, utadhania mwari wa harusi”
“Sasa huyo atapata kweli muda wa kupika ukimuoa?” nikamuuliza.
“Ndio maana nilishindwa kumuoa. Nilikuwa nikijiambia huyu msichana sijamuoa yuko hivi, je nikimuoa atakuwaje, piku kila siku…safari haziishi”
“Mapenzi ya kweli yana gharama” Yasmin akamwambia.
“Ni kweli lakini gharama ya mwanamke wa Mombasa ni kubwa. Kwanza kunai le gharama ya miraa. Kila siku ni lazima umnunulie kilo moja ya miraa, tena ile miraa safi ya bei ghali”
“Wacha we!” Yasmin alimwambia kumtia jazba.
“Halafu wkati wa kula ile miraa ni lazima apate kokakola na chupa ya maji safi pamoja na mfuko mzima wa Big G. Zote ni pesa” Masudi aliendelea kueleza.
“Na wewe ulikuwa unakula?” nikamuuliza.
“Mimi nilikuwa nakula lakini si sana. Simalizi hata nusu lakini mwenzangu anaua kilo nzima. Akianza saa tisa hadi saa nne usiku hakuna kitu”
“Sasa akishakula hiyo miraa itamsaidia nini?” Yasmin akauliza.
“Anapata handasi” Masudi akamjibu.
“Handasi ni kitu gani?”
“Handasi ni kileo cha miraa. Wengine wanakiongezea na kungumanga. Wanasaga kungumanga, ule unga wake wanachanganya na kahawa. Ashiki yake ni hatari!”
Sote tukacheka. Yasmin ndio alicheka sana.
“Yaani mwanamke akitoka hapo ni lazima apate bwana!” Masudi aliendelea.
“Asipopata bwana inakuwaje?” Yasmin akamuuliza.
“Yaani anapokula miraa na kuchanganya na kahawa ya kungumanga tayari anakuwa na ahadi ya bwana”
“Kwa hiyo huyo mpenzi wako akishakula ndio mnakutana?’ Yasmin aliendelea kumuuliza. Maneno yalikuwa yamemkolea.
“Ndiyo maana yake”
“Unaonaje mapenzi yake?”
“Ni mapenzi adhimu. Sijapata kuona na sitamsahau yule msichana” Masudi kwa kutaka sifa aliongeza. “Na yeye pia hatanisahau kwani nilikuwa…mh!..hata havisemeki”
“Sema tu ulikuwaje?” Yasmin akamsisitizia.
“Mwenyewe alikuwa akiniambia penzi nililokuwa nikimpa hajalipata kwa mwanaume yeyote”
Hapo tulicheka tena. Lakini mimi nilicheka kwa kujua kuwa Masudi alikuwa akisema uongo kumfurahisha Yasmin. Na kwa kweli nilihisi alitaka kujipependekeza naye ili apendwe yeye.
“Sasa ilikuwaje mkaachana?’ nikamuuliza.
“Tuliachana baada ya mimi kurudi Unguja. Mama yangu aliniambia nirudi kwa sababu alikuwa akiishi peke yake”
“Baba yako alikuwa yuko wapi?” Yasmin akamuuliza.
“Alikuwa ameshakufa”
“Nani ambaye hajaoa katika nyinyi?”
ITAENDELEA

SEHEMU YA 15

Wenzangu wote walikuwa na wake zao isipokuwa mimi lakini Masudi alisema alioa kisha aliachana na mke wake. Nilichokuwa nakijua mimi ni kuwa Masudi alikuwa na mke wake.
Sikujua ni kwanini Yasmin alituuliza vile.
“Kwa hiyo wewe na Masudi ndio hamna wake?” Yasmin akaniuliza.
“Ninachojua mimi Masudi anaye mke” nilimwambia Yasmin.
Kauli ile ilimkera Masudi.
“Nina mke mimi?” Masudi akaniuliza kwa ukali kidogo.
“Unaye!” nikamwambia kwa mkazo.
“Mke si nilishamuacha?. Au wewe ulikuwa hujui?”
“Mimi najua watania tu lakini mke bado unaye”
“Basi na yaishe. Mimi niliuliza tu kutaka kujua. Kama unaye mke au huna hakuna tatizo” Yasmin akaingilia kati.
“Huyu bwana mdogo anapenda sana kuniingilia!” Masudi akaunguruma.
Nikaamua kunyamaza.
“Nimesema yaishe jamani. Ngoja tulete karata tucheze”
SASA ENDELEA
Yasmin alitumia hekima kuyageuza yale mazungumzo akaenda kuleta karata, tukawa tunacheza.
“Hivi hizi karata ulikuwa unacheza na nani?” nikamuuliza Yasmin wakati tunacheza.
“Ninacheza na huyo aliyezileta”
“Harishi?”
“Ndiye huyo huyo. Anapoona nimepooza ananiambia kalete karata”
“Anajua kucheza karata?” akaulizwa na Masudi.
“Anajua. Hawa majini ni kama watu tu. Tofauti yetu ni ndogo sana. Wanafanya mambo mengi wanayofanya binaadamu”
Mazungumzo ya Harishi yalitufanya tukose amani. Yalitukumbusha wenzetu waliouawa. Mwenzetu mmoja lakini si Masudi akatuambia.
“Tuondoke twende kule tulikohamia”
“Chukueni hizo karata mwende nazo. Mtakwenda kucheza huko huko” Yasmin akatuambia.
Ilibidi tuondoke twende katika ile nyumba lakini Yasmin tulimuacha.
Tulipofika tuliendelea kucheza karata. Baadaye sote tulipitiwa na usingizi tukalala.
Tuliamshana jioni tukaamua tutoke twende tukatembee tembee. Tulizunguka sana katika kile kisiwa. Tulienda pia kuliangalia jahazi letu. Tuliporudi jua lilikuwalimeshakuchwa.
Tulimkuta Yasmin akitusubiri. Alikuwa ametuletea chakula cha jioni.
“Mnatoka wapi?” akatuuliza.
“Tulikwenda kutembea tembea kidogo” Masudi akamjibu na kuongeza “Kukaa tu kunachosha”
“Umetuletea chakula?” nikamuuliza Yasmin.
“Nimewaletea kabisa. Ikifika usiku sitaweza kuja huku. Harishi anaweza kuja wakati wowowte” Yasmin alituambia na kutuwekea chakula hicho juu ya meza.
“Ngoja nikusindikize” Masudi akawahi kumwambia Yasmin. Nilijua alitaka kunipiku mimi kwani alijua mimi ndiye ningemsindikiza.
Yasmin akakubali kuondoka na Masudi. Kwa upande wangi kitendo kile cha Masudi nilikiona kama ulimbukeni uliopitiliza na kutaka kujipendekeza kwa Yasmin.
Walipoondoka sisi tulikaa barazani mwa ile nyumba hadi giza likaingia.
“Mbona masudi harudi?” Tukawa tunaulizana.
Kusema kweli kitendo chake cha kuchelewa kurudi kilinikera. Nikaamua nimfuate peke yangu nijua alikuwa anafanya nini muda wote huo.
Nikaenda huku nikiwa na hasira. Nilipofika sikuingia ndani. Niliamua kufanya upelelezi kwa kuchungulia kwenye madirisha.
Wakati nachungulia niliana kusikia sautiya Yasmin ikiwa katika dhihaka, mwenyewe sikumuon. Nilibadilisha dirisha na ndipo nilipowaona wote wawili. Masudi alikuwa akikimbizana na Yasmin mle ndani kam waliokuwa wakicheza. Wakati mwingine Masudi alimkamata Yasmin na kuanguka naye chini akiwa amemshika kiuno.
“Kumbe wana mchezo huu, ndio maana amesahau kurudi” nikajisemea kimoyo moyo.
Licha ya moyo wangu kuuma nilijiambia chaguo la Yasmin ni mimi, Masudi alikuwa akijipendekeza tu.
Macho yangu yaliwashuhudia wakiwa wamelala chini. Masudi alikuwa kama akibembeleza kitu kwa Yasmin. Yasmin alikuwa ametulia akimsikiliza.
Sikuweza kufikiria chochote zaidi ya kuhisi kuwa Masudi alikuwa akimtongoza Yasmin na alikuwa akinifitini mimi.
Sikutaka tena kuuona upumbvu wake. Nikaamua kuondoka kwani usiku ulikuwa unazidi kushamiri.
Yasmin haweza kumkubali Masudi, Yasmin amenipenda mimi, nilijiambia kujifariji wakati naondoka.
Nilirudi kwa wenzangu huku nikiuzuia moyo wangu usitaharuki kutokana na kitendo kile nilichokiona kwa Masudi kumkumbatia Yasmin.
“Umemkuta?” Wenzangu wakaniuliza.
“Sikufika” nkawadanganya. “Nimeamua kurudi njiani, naona usiku mwingi huu”
“Au twendeni sote?” Mmoja akaniuliza.
“Tumsubirini tu hapa hapa”
Sikutaka kuwambia ukweli kuwa nilimkuta akifanya vitendo vya kipuuzi. Nilihisi wangeweza kuja kumwambia mwenyewe halafu kwa akili za Masudi tunaweza kugombana bure.
Tukakaa kumsubiri hadi saa tatu. Tulipoona hatokeai tuliamua kula chakula na kumbakishia chake.
Nilikuwa nimebaki na wenzangu wawili Shazume na Haji. Kwa upande wangu nilishakijua kilichokuwa kinamchelewesha Masudi lakini wenzangu walikuwa na wasiwasi kwamba huenda Masudi amepata matatizo.
Walikuwa wakisisitiza kuwa twende tukamuangalie.
“Kutoka usiku huu si vizuri” nikawambia. “Acheni tungoje kesho asubuhi tutakwenda kumuangalia”
ITAENDELEA

SEHEMU YA 16

“Kaka Masudi ana matatizo sana. Kwanza hatuelewi ni kitu kilichomfanya amsindikize yule msichana” Shazume akasema.
“Tusiwe na wasiwasi naye sana. Huenda mwenyewe ameamua kubaki” nikawambia wenzangu.
“Atabakije kule wakati anajua kuwa lazima Harishi atakuja?” Haji akauliza.
“Kila mtu ana akili yake jamani tusimuhukumu” nikawambia Shazume na Haji.
“Atajua mwenyewe, shauri yake” ilikuwa sauti ya kukata tamaa ya Haji.
Baada ya kujadiliana kwa kirefu tuliamua kwenda kulala. Kila mtu aliingia kwenye chumba chake.
Unapofika wakati wa kulala mawazo hubadilika. Fikira zote huondoka na kichwa kujaa mawazo ya Harishi.
Nilikuwa na hakika kuwa sikuwa mimi peke yangu bali wenzangu wote walikuwa na mawazo kama yangu. Likini hatukuwa na lolote la kufanya zaidi ya kukubali matokeo yatakayotokea usiku huo kwa Masudi.
SASA ENDELEA
Usiku ule tulilala na kuamka salama ingawa tulilala kwa mashaka.
Lakini Masudi hakuwa miongoni mwetu. Tukadhani kwamba atatokea wakati ule wa asubuhi baada ya kushindwa kurudi usiku. Lakini tulikaa hadi majira ya saa bila kumuona yeye wala Yasmin.
“Wenzangu mnaonaje twende tukamuangalie Masudi au tuendelee kumsubiri?” nikawauliza wenzangu.
“Kwenda kumuangalia ni jambo zuri lakini tunaweza kukutana na Harishi” Haji akasema.
“Nina wasiwasi kwa sababu Yasmin pia amekaa kimya. Kwa kawaida muda huu angekuwa ameshakuja” nikawambia wenzangu.
“Hatuwezi kujua lolote linaweza kuwa limetokea” Shazume naye akasema.
“Basi tusiende, tuendelee kusubiri hapa hapa hadi atakapokuja Masudi au Yasmin” nikawambia.
Wakati tunaendelea kujadiliana tulimuona Yasmin akiingia. Sote tukageuka na kumtazama. Kitu kilichotushitua si tu alikuwa peke yake bali macho yake yalikuwa mekundu yaliyoonesha alikuwa analia.
Akatusalimia na kutuambia kuwa amepatwa na fadhaa.
“Kwanini?” akatuuliza.
“Kaka yenu Masudi hakutumia busara hata kidogo” Masudi alituambia huku akitikisa kichwa kusikitika.
“Kwanini hakutumia busara?” nikamuuliza huku nikifikiria mengine. Nilifikiria ama Masudi alitaka kumbaka Yasmin au alimbaka kwani ile hali niliyowakuta nayo usiku uliopita haikuwa ya kawaida.
“Kama yeye amenipenda mimi kama alivyoniambia mwenyewe ni sawa lakini kitendo alichokifanya si kizuri kwa sababu anajua mimi nimemilikiwa na Harishi”
Hapo nilijua moja kwa moja kuwa Masudi amembaka Yasmin na ndio sababu alikuwa analia.
“Kwani amefanya nini?” nikamuuliza.
“Ungetueleza alichofanya” Haji naye akamwambia.
“Jana usiku nilimwambia arudi huku, ulikuwa ni usiku. Lakini alikataa kurudi, akataka kulala na mimi. Nilimsihi sana arudi lakini aligoma kabisa, tena alitaka alale na mimi chumba kimoja. Aliniambia ananipenda” Yasmin akatueleza.
“Masudi ni kaka yetu lakini ana matatizo sana” Shazume akadakia.
“Sasa ikawaje?” na mimi nikauliza kwa pupa.
“Nilimuachia alale. Yule ni mwanaume nisingeweza kumzuia”
“Ulilala naye chumba kimoja?” nikamuuliza.
“Nilimuomba sana akalale chumba kingine kwa usalama wake. Nilimwambia Harishi akija na kukukuta atakuua. Akakubali kwenda kulala chumba kingine”
“Sasa nini kimetokea?” Shazume akauliza.
“Harishi alikuja muda ule ule akamkuta ukumbini anazungukazunguka, akashikwa”
Alipofikia hapo Yasmin alianza kulia.
“Sasa ameuliwa?’ nikamuuliza.
“Harishi aliacha mtu siku gani?” Yasmin akaniuliza.
Mimi na Haji na Shazume tulitazamana tukiwa tumeacha midomo wazi.
“Aliyataka mwenyewe!” Yasmin akasema.
“Ni kweli aliyataka mwenyewe, kifo kilikuwa kinamuita” nikamuunga mkono.
“Angekuja kulala na wenzake pengine angenusurika” Yasmin aliendelea kutuambia.
“Mbona hukuja mapema kutuambia?” nikamuuliza.
“Harishi ameondoka sasa hivi. Jana usiku alipokuja alikuwa amelewa na alipomuua Masudi hakuondoka tena hadi hii asubuhi”
“Kumbe majini pia wanalewa?”
“Wanalewa kama watu. Harishi analewa sana”
“Hiyo pombe anaipata wapi?”
“Sijui mwenyewe”
“Na anapokuta mtu mle ndani anakuuliza ni nani?”
“Anaua kwanza halafu ndio anauliza. Mimi humwambia kwamba ni wavuvi wameingia kwa bahati mbaya. Lakini kama angenikuta nimelala naye angejua ni mwanaume wangu”
“Angekuua?”
“Sijui ingekuwaje?”
Pakapita kimya cha sekunde kadhaa. Sote tulikuwa tunamkumbuka kaka yetu Masidi.
“Mtanisamehe sikuwaletea chai. Nilikuwa nimetaharuki sana” Yasmin akatuambia baadaye.
“Misiba kama hii. Kila siku anakufa mtu. Hamu ya kula pia inapotea” nikamwambia.
“Nyinyi mtabaki huku huku mjaribu bahati zenu. Mnaweza kusalimika”
ITAENDELEA