Kwa sababu hatuvioni ndani mwetu, hatuwezi kuwapa wengine!

Kuna nyakati za magumu na upweke ambazo hutufunza. Ni zile nyakati ambazo unajihisi ukiwa mpweke na kutengwa. Ukihisi ya kuwa hakuna hata mmoja anayekusikiliza. Unapata hisia kuwa upo peke yako japokuwa wapo watu wengine unaoishi nao na licha ya kuwa unatambua kuwa dunia imejaa watu wengi na viumbe wengi wanaokuzunguka.

Ni kweli kuwa licha ya kuwa dunia imezunguka, ni wewe ndiye uijazayo na unayeisanifu. Wewe kama nafsi watosha. Na unabaki wakati ambao aliyebaki kwako ni Mungu.

Nyakati hizi hutokea pale unapokuwa unajihisi kuwa umekosa kitu (vitu) ulichokihitaji maishani, na hata wakati unapohisi kuwa una kila kitu ulichokihitaji maishani mwako. Pia huja katika nyakati ambazo karibu kila kitu ulichokuwa nacho umekipoteza ama umepewa kila kitu ambacho ulikipoteza.

Nyakati hizi zinapofika, ni nyakati za kupona na kuachia majeraha mengi ambayo yalikuwa yakikurudisha nyuma kwa muda mrefu maishani mwako. Na ni nyakati za uvumbuzi wa chemchem ndani mwako. Ni kipindi cha giza kiletacho mwanga.

Na katika nyakati hizi bado kuna kitu muhimu ambacho moyo wako unakihitaji sana na ambacho wengi hukitafuta kwa muda mrefu maishani, ni kupendwa kwa dhati na kuthaminiwa.“Je, kuna yeyote anayenipenda na kunithamini kwa dhati jinsi nilivyo?” Ni maswali ambayo utajiuliza sana katika nyakati hizi za ugunduzi.

Tumekuwa tukidhani kwamba tunaweza kupata upendo wa dhati na thamani ya kweli toka kwa wengine. Tumetafuta kwa muda sana upendo toka kwa ndugu, marafiki na majirani. Tumetafuta kwa wale tuliowaamini kwa dhati na mara nyingi kuishia kwenye kuumia.

Tukaingia kuutafuta upendo na thamani ndani yetu lakini mara nyingi tumeshindwa kuupata. Hivyo kushindwa kuutambua ndani mwetu kumetusababisha kushindwa kutoa kwa wengine. Na kwa vile tumeshindwa kuupata kwetu tumeutafuta tunapodhani upo, tunaukosa na kuishia kuogopa kuweka matumaini yetu huko tulipodhani upo.

Na hivyo ndivyo itokeavyo, tunatafuta pale ambapo hatukuhifadhi. Na kama hatukuuweka upendo popote vivyo hivyo hatuwezi kuupata. Kile ambacho hatukitoi maishani hatuwezi kukipata kwa sababu hapa duniani sisi ndio wasanifu na wabomoaji.

Kama tunakosa kusamehewa, ni kwa sababu hatukupata kusamehe. Kama hatuthaminiwi ni kwa sababu hatukupata kuijenga thamani sisi wenyewe. Kama hatuvumiliwi, ni kwa sababu hatukujenga uvumilivu sisi wenyewe. Kama hatupati haki na usawa ni kwa sababu hatukuanza kuijenga ndani mwetu. Kama hatuupati upendo, basi ni kwa sababu hatukupata kuujenga upendo ndani mwetu. Na kama hakuna ambaye anapata thamani toka kwa wengine, ni kwa sababu hatukuanza sisi kuijenga ndani mwetu.

Mambo yote haya ni lazima yaanze ndani kwetu sisi kisha yaende kwenye maisha ya wengine. Lakini kwa sasa hatuuoni uzuri uliopo ndani mwetu uliojazwa na uzuri wa Muumba. Hatuoni uaminifu ndani mwetu. Hatuoni usafi ndani mwetu.

Kwa sababu hatuvioni hivi vyote ndani mwetu, hatuwezi kuwapa wengine. Lakini pia kwa sababu si kwamba sisi ni vipofu mioyoni mwetu, tunaviona kwa wengine na kuvihitaji tusitambue kuwa tunavyo. Ni mara nyingi tunaona upendo kwa wengine, tunaona huruma kwa wengine, tunauona usafi wa moyo kwa wengine, tunayaona matumaini kwa wengine. Hivyo kwa kuviona kwa wengine, tunajaribu kutenda kwa baadhi yao lakini si ndani mwetu. Mara nyingi tunashindwa kwa sababu ya vidonda tulivyonavyo.

Kwa sababu ya vidonda tulivyonavyo, tunashindwa pia kutibu majeraha ya wengine. Hivyo hatuthamini jinsi dunia inavyotuhitaji kila mmoja kwa nafsi yetu.Tunashindwa kutambua kuwa dunia inahitaji kile kitokacho ndani mwetu ikiwemo upendo, usawa, haki, thamani kwa wengine, uvumilivu na kujitolea. Tunaishia kuilamu dunia tusijue kuwa ni sisi ndio tulioanza kuisanifu. Na hivyo tunaweka picha ndani mwetu kuwa dunia ni mbaya na onevu tena sehemu ya kupita kwa machungu.

Hatuwezi kupata kutoka katika dunia vile ambavyo hatukuvipanda. Na sasa tunapaswa kukumbuka hapa kuwa: Chochote ambacho hatukukipanda duniani, hatuwezi kukivuna katika dunia hiyohiyo. Tunavuna tulichopanda.Hapa ndipo unapokuja wakati tunapogundua kuwa sisi ndio wasanifu wa dunia na kila kilichomo. Ni wasanifu wa maisha ya leo na ya kizazi kijacho. Hakuna atakaye tupatia chochote kile ambacho hatukuanza sisi kukipanda na kukitoa kwa dunia hii tuishimo. Na mara nyingi tunamuomba Mungu na wakati mwingine kumlaumu kwa kutotupatia kile ambacho hatukuanza sisi kukitengeneza na hata kukitoa kwa wengine pale tulipostahili kufanya hivyo.

Kama huwezi kumsamehe unayeishi nae, unashindwa kumpenda, kuishi nae kwa amani na uhuru na hata kumvumilia, ni vigumu kutarajia kupata kutoka kwa huyohuyo unayeishi na kulala naye. Upendo, thamani, uvumilivu, uhuru, amani na thamani ya kweli. Tutapata kadiri tulivyotoa.

Huwa tunafikiri kuwa ndani ya mahusiano, mwenzi atakupatia vitu ambavyo unajihisi huna. Tunadhani tutapata upendo ambao sisi hatuutoi, msamaha ambao sisi wenyewe hatuutoi. Huu ni moja ya uongo mkubwa tunaojidanganya ndani ya nafsi zetu.

Tunapotamani kupatiwa pasipo kutoa, mwisho wake kila kitu hufifia, kisha chuki huingia na kisha mahusiano hufa. Kisha tunagundua kuwa ni sisi wenyewe tulijidanganya. Sasa tunatambua kuwa hakuna pa kukimbilia zaidi ya Mungu. Tunarudi kwa Mungu na kumwambia… “Tafadhali Mungu wangu naomba unisamehe. Naomba unijalie amani na upendo, nijalie uvumilivu na moyo wa kujitolea. Nakuomba baba unijalie hivi nami niwagawie wenzangu.”

Kila nafsi ijifunze kupanda na kutaraji mavuno. Kila nafsi iithamini nafsi nyingine na kila nafsi itambue kuwa inahusika kujenga dunia mpya na isiwe tayari kulaumu dunia na kuidai dunia kile ambacho haikukipanda wala kukitoa. Kisha dunia itakuwa sehemu bora ya kuishi…

Ahsante kwa yote. Barikiwa.

hata kama nimdhaniaye hatonirudishia ninachokitoa kwake,yuko nisiyemdhania atanirudishia hata kama sikumpa yeye.

Sorry ndefu mno

Madini matupu

Ooh, samahani nimejaribu kuifupisha lakini nikaona inapoteza maana. Wakati mwingine tuvumiliane…

madini yaliyotukuka, hatuishi kujifunza hasa ukiamin ya kua una ving huvijui, kuna walioishia katkat, kuna ambao hawajasoma kbsa na kuna waliosoma mwanzo mwisho, hapo ndo tunatofautiana na hapo ndo raha ya dunia na watu wake ilipo na ngoma ndo huchezewa hapo

NOTE: kusoma na kuelewa n vitu viwil tofaut.

sawa mzee wa kijiji

Ngoja nitamalizia kusoma badae