The world has no equality

ERIC SHIGONGO
DUNIA HAINA USAWA

“Mkuu! Kuna taarifa kutoka nchini Ubelgiji!” alisikika mwanamke akizungumza kwenye simu.
“Taarifa gani?” aliuliza Ojuku.
“Bokasa ametoroshwa hospitalini!” alisema mwanamke huyo.
Ojuku akashtuka, akasimama pale alipokuwa, akauliza tena juu ya kile alichoambiwa, alihisi kama hakusikia vizuri, kilekile alichoambiwa ndicho akaambiwa kwa mara nyingine kwamba Bokasa alikuwa ametoroshwa hospitalini na kulikuwa na taarifa kwamba gari lililokuwa limemsafirisha lilionekana uwanja wa ndege.
Hakutaka kusikia lolote lile, haraka sana akapiga simu mpaka nchini Ubelgiji na kuzungumza na waziri mkuu wa nchi hiyo na kumwambia kilichokuwa kimetokea, waziri huyo yeye mwenyewe alishangaa kwani kitu kama hicho hakikuwa kutokea nchini mwake, ilikuwaje mpaka mgonjwa atoroshwe huku madaktari wakiwa hawafahamu chochote kile.
Simu ikapigwa mpaka hospitalini ambapo akathibitishiwa taarifa hiyo na hivyo kuzungumza na kamanda mkuu wa jeshi la polisi nchini humo na kumwambia kwamba alitakiwa kupambana mpaka kuhakikisha anafahamu mahali mgonjwa huyo alipopelekwa.
Ndani ya dakika kumi tu akapewa taarifa kwamba gari lililokuwa limemchukua lilionekana uwanja wa ndege hali iliyoonyesha kwamba mtu huyo alitakiwa kusafirishwa kuelekea nchi fulani.
“Mtafuteni hapo! Jueni hilo gari limempeleka hapo kwa lengo la kwenda wapi! Hakutakiwi ndege yoyote kuondoka mpaka tujue huyo mgonjwa alikuwa akipakizwa ndani ya ndege gani. Hakikisheni hakuna ndege inayoondoka muda huu!” alisikika kamanda mkuu wa jeshi la polisi nchini humo.
“Sawa mkuu!”


Wilson akawasiliana na Olotu na kumwambia kwamba mtu waliyetumwa waende kumchukua tayari alikuwa mikononi mwao na wakati huo walikuwa njiani kuelekea uwanja wa ndege. Hiyo ilikuwa taarifa nzuri, na kwa sababu ndege ya rais ilikuwa imekwishafika katika uwanja huo, akawaambia kwamba hakukuwa na tatizo lolote lile, walichotakiwa ni kufika uwanjani hapo na kuondoka na mtu huyo.
Walipofika, gari likapitishwa mpaka ndani kabisa ya uwanja huo, walipewa taarifa kwamba kulikuwa na ndugu wa rais ambaye alipelekwa katika hospitali moja hapo Brussels kutibiwa na alikuwa amepona hivyo kutakiwa kurudishwa nyumbani. Hata Bokasa alipoteremshwa huku akiwa kwenye kiti chake, hakukuwa na mtu aliyekuwa na hofu kwa kuhisi kwamba huyo alikuwa ndugu wa rais wa Kenya.
Hakukuwa na muda wa kupoteza, kila kitu kilikuwa tayari na kilichofanyika kilikuwa ni kuingia ndani ya ndege na hapohapo kuwashwa tayari kwa kuondoka nchini Ubelgiji. Kila mmoja akashusha pumzi, kazi nzito waliyokuwa wamepewa waliikamilisha kwa kiasi kikubwa na hapo walikuwa wakielekea nchini Kenya kwa ajili ya kumkabishi Bokasa katika mikono ya Olotu aliyehitaji kujua kitu kimoja tu, majina ya wafanyabiashara waliokuwa wamepewa mzigo mkubwa wa madawa ya kulevya.
“Koh koh, koh! Nyie ni wakina nani?” alikohoa Bokasa na kuuliza, alikuwa akiwaangalia wanaume hao, mpaka kipindi hicho hakujua kilichokuwa kikiendelea, aliwaona watu wakiwa wameingia ndani ya chumba kile kama madaktari, wakamchukua, wakampakiza ndani ya ndege na kuondoka.
“Utatufahamu! Kwa kifupi ni kwamba tumetumwa kuja kukuchukua,” alijibu Wilson huku akimwangalia mwanaume huyo.
“Na nani?”
“Olotu! Unamfahamu?” alidakia Okotee huku akiwa amemsogelea Bokasa karibu na kitanda chake.
Alimfahamu mtu huyo, alikuwa mmoja wa marafiki zake ambao alikuwa akishirikiana nao katika mambo yake machafu. Kitendo cha kumchukua kule Ubelgiji hakikuwa kumpenda sana bali kulikuwa na jambo jingine kabisa ambalo alitaka kulifanya kwa ajili ya kupata kitu fulani kutoka kwake.
Hakuwa na furaha, alijua dhahiri kwamba alitoka mikononi mwa maofisa wa Usalama wa Taifa lakini katika mikono aliyokuwa ameangukia, hakukuwa na amani hata mara moja. Akabaki kimya, akaanza kuyakumbuka majina ya watu aliokuwa akiwauzia madawa ya kulevya, aliyakumbuka majina yote matatu ambayo alitakiwa kuyataja kama tu angefika nchini Kenya na kuulizwa kuhusu watu hao.


Gari la wagonjwa lilikuwa likionekana katika uwanja wa ndege, kila mmoja alikuwa na uhakika kwamba inawezekana mtu waliyekuwa wakimtafuta alikuwa ndani ya gari hilo. Polisi wanne wakalisogelea huku wakiwa na bunduki mikononi mwao, walipofika, wakafungua mlango, ndani hakukuwa na mtu yeyote yule.
Hilo likawachanganya, hawakubaki mahali hapo, wakaondoka mpaka katika ofisi ya meneja wa uwanja huo na kumuuliza kilichokuwa kimetokea kwamba waziri mkuu alisema kwamba hakukutakiwa ndege yoyote kuondoka kwa kuwa kulikuwa na mtu aliyekuwa akitoroshwa, kwa nini sasa mtu ateremshwe kutoka mule, apandishwe ndani ya ndege na kuondoka?
“Tangazo lilichelewa kutoka. Nilipigiwa simu saa 7:30, wakati nikipigiwa simu hiyo, ndege iliyomchukua ndugu wa rais kutoka katika gari lile iliondoka saa 7:15. Sasa ningefanyaje?” alihoji meneja huku akiwaangalia polisi waliokuwa wameingia ofisini kwake.
Tatizo halikuwa kwake, alifanya kile alichoagizwa kufanya ila tatizo hilo likahamia kwa Dk. Thump ambaye yeye na madaktari wenzake walifanya uzembe mkubwa mpaka kutokuona wakati Bokasa akiondolewa ndani ya chumba kile na kupelekwa uwanja wa ndege.
Uzembe huo ukaanza kutangazwa kila kona, watu wakatoa taarifa katika mitandao ya kijamii kwamba Bokasa aliyekuwa rais wa Tanzania alitoroshwa nchini Ubelgiji kwa kutumia ndege ya rais wa Kenya na kupelekwa sehemu isiyojulikana.
Taarifa za ndege ya rais kutumika katika utoroshaji wa Bokasa nchini Ubelgiji zikapingwa vilivyo na msemaji wa ikulu ambaye aliwataka watu wote wasiziamini taarifa hizo kwa kuwa kulikuwa na ugomvi uliokuwa ukiendelea chini chini baina ya Kenya na Ubelgiji.
“Hakuna kitu kama hicho. Ni stori ambazo zimesambazwa kwa kuwa kuna kitu kinaendelea! Hatuwezi kumtorosha mtu, tumtoroshe kwa maslahi ya nani?” alihoji msemaji wa ikulu kauli iliyofanya watu kuhisi kwamba hakukuwa na kitu cha kweli kama hicho.


Ulikuwa ni kama ugomvi baina ya Tanzania na Kenya, hakukuwa na kitu ambacho Ojuku alikuwa akikihitaji kipindi hicho kama Bokasa aliyekuwa akisubiri kusafirishwa kupelekwa nchini Tanzania na kusomewa kesi yake iliyokuwa ikimkabili.
Mawasiliano yalifanyika baina ya nchi hizo, bado Kenya walikuwa wakisisitiza kwamba taarifa zilizokuwa zimetolewa hazikuwa za kweli, kulikuwa na mtafaruku uliokuwa ukiendelea baina ya Kenya na Ubelgiji baada ya nchi hiyo kuamua kubinafsisha mashamba yaliyokuwa yakimilikiwa na Wabelgiji hapo Kenya.
“Hapana! Kutakuwa na kitu! Haiwezekani taarifa hizo ziwe za uongo na wakati ndege imepigwa mpaka picha,” alisema Ojuku.
“Hutakiwi kuamini kila kitu unachokiona kwenye mitandao!” alisikika Rais Onyango.
“Kweli?”
“Ndiyo!”
“Hebu rudia nisikie tena!”
“Hutakiwi kuamini kila kitu unachokiona kwenye mitandao!” alisema kwa mara nyingine.
“Basi sawa. Ila usije ukaamini kitu kingine kinachotokea huko kwenye mitandao. Kuna siku utaniuliza, nitakwambia maneno hayohayo uliyoniambia! Umesikia?” alisema Ojuku na kuuliza swali.
“Nimesikia! Ila hutakiwi kuamini kamwe!” alisema rais huyo kwa kebehi na kisha kukata simu.
Ojuku akatulia, kichwa chake kilikuwa kikimuuma, moyo wake ulichanganyikiwa, Watanzania hawakutaka kusikia kitu chochote kile, mtu waliyekuwa wakihitaji kumuona nchini mwao hakuwa mwingine bali ni Bokasa tu ambaye mpaka kipindi hicho hakujulikana mahali alipokuwa.
Hakujua kipi alitakiwa kufanya. Wakati akiwa amekaa akifikiria mambo mengi mara akasikia simu yake ya mkononi ikipigwa, haraka sana akaichukua na kuangalia mpigaji, namba ilikuwa ngeni, hapohapo akaipokea.
“Halo!”
“Unazungumza na Godwin hapa,” alisikika mwanaume wa upande wa pili.
“Godwin! Umepiga simu wakati sahihi kabisa. Kuna kitu nataka unisaidie!” alisema Ojuku.
“Haina shida. Kabla hujaniomba, nimekwishajua hivyo nitakusaidia,” alisikika Godwin maneno yaliyomfanya Ojuku kushtuka kwani aliamini kwamba kila kitu alichokuwa amekizungumza kwenye simu kilikuwa baina yao watu wawili, iweje mwingine asikie kila kitu.
“Umesikia nini?”
“Nataka rais wa Kenya asiamini kila kitu anachokiona kwenye mitandao. Unaonaje?” aliuliza Godwin.
“Sawasawa. Ninataka maneno aliyoniambia ndiyo nimwambie,” alisema Ojuku.
“Basi sawa. Nipe saa kumi, kabla ya ndege kufika nchini Kenya, tayari kuna mambo yatatokea hapo Kenya, atagundua kwamba anacheza na watu hatari sana. Kama Usalama wa Taifa wa Uswisi walisumbuka sana, Wakenya watajificha vipi mpaka wasisumbuke. Nipe saa kadhaa tu! Kila kitu nitakiweka wazi,” alisema Godwin na kukata simu.


Ndege ilikuwa ikiendelea na safari kuelekea nchini Kenya, kila mtu alikuwa na amani moyoni mwake, walikuwa na uhakika kwamba wangefika salama nyumbani. Ndani ya ndege walikuwa wakiongea yao huku wakijipongeza kwamba walifanya kazi nzuri.
Marubani wawili, Sosi Omog na Amrani Neta walikuwa wakiendesha ndege huku wakifanya mawasiliano na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai kwa ajili ya kufika hapo, kuweka kituo kwa dakika kadhaa, kujaza mafuta na kuendelea na safari yao mpaka jijini Nairobi nchini Kenya.
Ndege ilichukua saa kadhaa mpaka kuficha Dubai ambapo ikatua, wakapumzika, wakajaza mafuta na kuondoka mahali hapo huku wakitakiwa kuunganisha moja kwa moja mpaka katika Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta nchini Kenya.
Ndege ilikuwa ikikata mawingu. Kila mmoja alitegemea kuingia jijini Nairobi baada ya saa kumi lakini kitu cha kushangaza kabisa, mpaka saa kumi na mbili zinakatika ndege haikuwa imetua katika uwanja huo jijini Nairobi.
Hilo likawatia wasiwasi Wilson na Okotee, wakajua kwamba kulikuwa na tatizo lililokuwa limetokea, walitaka kujua sababu ambayo iliwafanya rubani kuwa wazembe mpaka ndege hiyo kutokutua kwa wakati katika uwanja huo.
Wakawafuata na kuanza kuzungumza nao lakini watu hao wakawaambia kwamba kila kitu kingekwenda kama kinavyotakiwa, baada ya dakika kadhaa wangetua katika uwanja wa ndege.
“Sawa,” aliitikia Wilson.
Baada ya dakika arobaini na tano wakaambiwa wafunge mikanda yao kwani ndege hiyo ilikuwa ikijiandaa kutua katika uwanja wa ndege, wakafanya hivyo haraka sana na ndege hiyo kuanza kutua katika uwanja huo.
“Hatimaye tumefika. Mungu ni mwema,” alisema Wilson wakati ndege ikitembea katika ardhi ya uwanjani hapo na mbele kabisa kusimama.
Wakanyanyuka, mhuhdumu mmoja akaufungua mlango, gari lililokuwa na ngazi kubwa ya kushukia likasogea pale mlango wa ndege ulipokuwa, ukafunguliwa na kila mmoja kutakiwa kutoka ndani ya ndege hiyo. Wakamchukua mtu wao na kwenda mlangoni, walipoangalia nje, kulionekana kuwa tofauti, haukuwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta walioufahamu bali ulikuwa uwanja mwingine kabisa.
“Bumba Airport,” alisema Wilson huku akiwa amesoma ubao mmoja mkubwa ulioandikwa maneno hayo kiasi kwamba wakabaki wakishangaa.
“Bumba?” aliuliza Okotee huku naye akisogea mlangoni kuangalia kile alichokisikia.
“Ndiyo! Mbona tumeletwa Kongo badala ya Nairobi?” aliuliza Wilson huku akishangaa, hapohapo akaanza kuelekea kule mbele kuwauliza marubani ni kitu gani kilikuwa kimetokea, walipofika kule, cha kushangaza wakawakuta marubani wote wawili walikuwa wakilia kama watoto wadogo.


Godwin aliona kazi kubwa mno mbele yake, kichwa chake kilitakiwa kufanya kazi ya ziada kuhakikisha kwamba Bokasa anapatikana haraka iwezekanavyo. Kitu cha kwanza kabisa alichokuwa akihitaji kufanya ni kuhakikisha kwamba anapata majina ya marubani wa ndege ile ya raisi kwa ajili ya kufanya kazi aliyokuwa akiitaka.
Akawasiliana na Ojuku na kumuomba namba ya Rais Onyango, hilo halikuwa tatizo, namba hiyo ilikuwepo na hapohapo akampa. Godwin akachukua kompyuta yake na kuiingiza namba ile katika kuifungua prorgamu yake aliyoitengeneza kwa ajili ya kudukua namba za simu.
Alipoiingiza, likatokea neno ‘download’ huku mbele yake kukiwa na asilimia zilizokuwa zikipanda. Zilipanda na kupanda, kuanzia 0, 20, 37, 79 mpaka kufikia mia moja na hapohapo likatokea neno jingine yaliyosomeka ‘hacking process’ ambapo mbele yake kulikuwa na asilimia kama zile zilizokuwa zimepita.
Ilipofika mia moja, neno sehemu ile ikajiandika ‘hacking completed’ na hapohapo kuingia katika simu ya Rais Onyango na kuanza kuangalia kila kitu kilichokuwa humo. Akasoma meseji zote zilizoingia na kutoka, akagundua ukweli kuwa mpango mzima wa kumtorosha Bokasa haukuwa chini ya Onyango tu bali kulikuwa na mtu aliyeitwa Olotu, bilionea aliyekuwa akiishi kifahari Mombasa ambaye alimtaka mtu huyo kwa kuwa kulikuwa na wafanyabiashara aliofanya nao biashara ya kuuza madawa ya kulevya hivyo alihitaji majina ya watu hao.
Mpaka kufika hapo akapata uhakika wa kukamilisha kazi hiyo, akachukua simu yake na kumpigia Ojuku, akampa taarifa juu ya kile alichokuwa amekisoma kwenye meseji zile kwamba mtu aliyekuwa katika mpango mzima alikuwa Olotu ambaye aliitumia ndege ya rais kwa makubaliano maalumu.
“Ninamfahamu mtu huyo. Ni bilionea mkubwa sana, ana nguvu mno hapo Kenya,” alisema Ojuku kwenye simu.
“Huyo ndiye aliyehusika kwa kila kitu,” alisema Godwin.
“Duh! Sawa. Na vipi kuhusu kumpata mtu wetu?”
“Nipe saa moja kila kitu kitakuwa tayari,” alisema Godwin na kukata simu.
Bado kompyuta yake ilikuwa katika simu ya Rais Onyango. Alikuwa akiangalia kila kitu kilichokuwa kikiendelea. Akaenda kwenye majina ambapo huko akakuta majina mawili yakiwa yameandikwa Pilot Sosi na nyingine iliandikwa Pilot Amrani, akajua kwamba hao walikuwa marubani wa ndege yake.
Hakutaka kuchelewa, akazichukua namba zao na kuanza kuzidukua kwa kuingia kwenye kompyuta. Haikuwa kazi kubwa, ndani ya muda mchache akaingia ndani ya simu zao na kuchukua namba za wake zao, akaziunganisha na namba yake, akazidukua kwa lengo la kuwachezea mchezo mmoja hatari.
“Winfrida! Kuna kitu nataka unisaidie,” alisema Godwin huku akimwangalia mpenzi wake.
“Kitu gani?”
“Kuna watu nataka uzungumze nao. Ninahitaji udanganye kwamba wewe ni wake zao, uzungumze nao huku ukilia kwamba umetekwa na watu waliokuwa na bunduki ambapo kama hawatofanya kitu wanachokitaka basi unaweza kuuawa,” alisema Godwin.
“Kwa nini sasa?”
“Utajua baadaye! Unaweza kufanya hivyo?”
“Ndiyo!”
“Kwa lafudhi ya Kikenya, na wakati mwingine zungumza Kiingereza, usitoke nje ya biti! Yaani uwe kama Mkenya!” alisema Godwin.
“Hakuna tatizo!”
Alimuandaa Winfrida kwa ajili ya kuifanya kazi hiyo, hakuwa na hofu, alijua kwamba kwa namna moja au nyingine ilikuwa ni lazima kwa marubani wale kuamini kwamba walikuwa wakizungumza na wake zao. Kilichofuata ni kuanza kuwapigia simu, katika kila nchi waliyokuwa wakipita walikuwa na namba zao, Godwin alizichukua, na kwa kuwa aliambiwa muda ambao ndege hiyo iliondoka nchini Ubelgiji, akajua muda ambao ingetua Dubai na hivyo kujiandaa kuwapigia simu wakati ndege hiyo itakapotua nchini humo na kuzungumza nao.
Kila wakati alikuwa akipiga simu zao kujua kama walikuwa wamefika au la. Aliendelea hivyohivyo huku msichana wake akiwa pembeni yake akiwa amejiandaa kabisa kufanya kazi aliyotakiwa kuifanya. Dakika zilikatika, baada ya saa kadhaa alipojaribu kupiga simu ya Sosi, ikapokelewa na mwanaume huyo.
“Halo mke wangu!” alisikika mwanaume huyo kimapozi kabisa.
“Mume wangu njoo utuokoe! Mume wangu tunakufa, wanatuua…they want to kill us…pleasee come to save us…” alisema Winfrida kwa lafudhi akihitaji msaada wa kuokolewa kutoka kwa watu waliowateka, tena hakuzungumza hivihivi, alijifanya kulia kiasi kwamba ilikuwa vigumu kugundua kwamba hakuwa yeye.
“Nani amekuja wateka? Mke wangu! Who kidnapped you?” aliuliza Sosi huku akiwa amechanganyikiwa, hata kabla hajajibiwa kile alichokitaka, simu ikakatwa.
Alichanganyikiwa, akapiga simu kwa mke wake, kwa kuwa tayari Godwin alikuwa amekwishaidukua simu hiyo, ilipopigwa kwenda kwa mke wa Sosi, ikaingia kwake, akaipokea na kuipeleka sikioni.
“Halo! Mke wangu…mke wanguuuuu…” aliita Sosi.
“Nisikilize bwana mkubwa. Tupo na mke wako, tunamuua. Si yeye tu bali tupo na watoto wako pia, wote tunawaua. Ukifika huku, utakuta vichwa vyao katika jokofu na runingani kote wataitangaza habari hii,” alisema Godwin na kukata simu, alichokifanya ni kuifunga simu ya Sosi ili isitoke kwenda kwenye simu nyingine yoyote ile.
Hakuishia hapo, alipomalizana na Sosi akahamia kwa rubani Amrani na kumwambia vilevile. Marubani wote hao walichanganyikiwa, hawakujua kilichokuwa kikiendelea. Walizipenda familia zao, kwao, hizo zilikuwa kila kitu.
Walikuwa ndani ya ndege, maisha yao yalikuwa humo, walisafiri kwenda nchi mbalimbali na hata katika safari hiyo waliagizwa na rais kwa kuwa kulikuwa na mtu waliyetakiwa kwenda kumchukua, hivyo wakaenda peke yao pasipo watu wa rais ambao mara kwa mara walikuwa wakisafiri nao.
Kila mmoja akajua kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wa kuziona familia zao, wakawapigia simu, hazikutoka, wakati wakijifikiria ni kitu gani walitakiwa kufanya, mara simu ya Sosi ikaanza kuita na alipoipokea, Godwin akaanza kusikika.
“Nisikilizeni. Kuna jambo moja tu mtatakiwa kufanya ili kuzikuta familia zenu zikiwa salama kabisa,” alisema Godwin.
“Jambo gani? Tuambie, kitu chochote kile tutafanya. Kitu chochote kile,” alisema Sosi, Amrani akaona kama angeulizwa sababu ya yeye kutokuuliza, na hivyo kuuliza kama mwenzake.
“Ipelekeni ndege nchini Kongo katika Uwanja wa Ndege wa Bumba ambapo huko mtatakiwa kusubiri kuona kitakachotolewa. Mkiifikisha ndege huko tu, familia zenu zitakuwa salama ila mkileta mchezomchezo, mtavikuta vichwa vyao katika jokofu,” alisema Godwin kwa mkwara mzito.
“Sawa. Tunafanya hivyo!”
Hilo lilikuwa agizo, walijua kwamba ndege ilikuwa ni ya rais wa Kenya lakini ilikuwa ni lazima ipelekwe nchini Kongo kama tu walihitaji kuziona tena familia zao zikiwa salama kabisa. Hakukuwa na haja ya kujadili kitu chochote kile, hawakuwaambia Wilson na mwenzake kilichotokea bali walichokifanya ni kuwasha ndege na kuelekea nchini Kongo.
Njiani, kila mmoja alikuwa na huzuni, waliogopa, walihisi kabisa kwamba mtu aliyekuwa amewapigia simu kulikuwa na uhakika kwamba alikuwa Al Shaabab hivyo kama wasingefanya kile kilichotakiwa kufanywa basi wote wangeuawa kama walivyoambiwa.
Safari ikawa chungu, ikaendelea mpaka walipofika katika uwanja huo ambapo watu wa anga walionekana kuwa na taarifa kwamba ndege ya rais wa Kenya ingetua katika uwanja huo kitu kilichowashangaza kwamba kwa nini isingekwenda kutua Kinshasa au Lubumbashi mpaka wakaamua kwenda Bumba?
Ndege ilichukua saa kadhaa, ikaanza kutua katika uwanja huo wa ndege ambapo hata kabla Wilson na Okotee hawajateremka wakaona kundi la wanajeshi zaidi ya hamsini kutoka nchini Tanzania wakiingia na bunduki katika uwanja ule huku wakiifuata ndege ile.
“Washeni ndege tuondoke! Kwa nini mmeileta ndege hii huku?” aliuliza Wilson huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Kwa sababu ya familia zetu. Tumefanya hivi kuziokoa familia zetu,” alijibu Sosi huku mashavu yake yakiwa yamelowanishwa kwa machozi yaliyokuwa yakimtoka mfululizo.
“Familia zenu?”
“Ndiyo! Tusingefanya hivi, zingeuawa,” alijibu Amrani, hapohapo wakawasikia wanajeshi wale wakianza kupandisha ngazi za ndege ile na kuingia ndani. Wakawekwa chini ya ulinzi na Bokasa kuanza kuteremshwa huku akiwa katika kitanda maalumu.
“Bokasa! Karibu sana katika mikono ya Watanzania. Upo salama, tunakupeleka nchini kwako, kuna kesi nyingi zinakusubiri,” alisema mwanajeshi mmoja aliyekuwa na kofia iliyokuwa na rangi ya damu ya mzee.
“Jamani! Mbona sielewi?”
“Utaelea tu baada ya kufika katika Mahakama ya Kuu! Mpelekeni chini,” alisema mwanajeshi huyo na hapohapo kuanza kushushwa kibabe.


Godwin ndiye aliyeanzisha maneno maneno katika Mtandao wa Instagram, aliandika kwamba ndege ya Rais wa Kenya ilikuwa imepotea katika mazingira ya kutatanisha na tayari ilionekana angani ikienda katika nchi fulani Afrika.
Habari hiyo ndiyo iliyoanza kusambaa mpaka ilipowafikia Usalama wa Taifa nchini kenya ambao moja kwa moja wakawasiliana na Rais Onyango na kumwambia kilichokuwa kimetokea.
Hilo lilimchanganya mno, hakuamini kilichokuwa kimetokea, alihisi kwamba ulikuwa ni uongo, akawapigia simu watu wa anga uwanja wa ndege ili kupata taarifa ya ndege hiyo na wao kumwambia kwamba hakukuwa na dalili za ndege hiyo kutua siku hiyo kwani kama kulikuwa na ratiba hiyo basi wangepewa taarifa wakati ndege ikiondoka Dubai.
“Tanzania!” hilo ndilo jina lililomjia kichwani mwake. Haraka sana akachukua simu na kumpigia Ojuku, akagundua kabisa kwamba mwanaume huyo alifanya kitu kimoja mpaka ndege hiyo kupotea katika mazingira ya kutatanisha. Simu ilipopokelewa, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumwambia kilichokuwa kimetokea na alikuwa na uhakika kwamba alihusika katika hilo.
“Kwani taarifa hizo umezipata wapi rafiki yangu?” aliuliza Ojuku.
“Watu wangu wamezipata Instagram kwenye akaunti ya Mabadiliko ya Kweli!” alijibu Rais Onyango huku akitetemeka.
“Nisikilize Onyango. Hutakiwi kuamini kitu chochote unachokiona katika mitandao. Au umesahau hilo?” aliuliza Ojuku swali lililomfanya Rais Onyango kupandwa na hasira kali.


Rais Onyango alikasirika, jibu alilopewa na Ojuku kumwambia kwamba hakutakiwa kuamini taarifa zilizokuwa katika mitandao lilimkera. Hakutaka kuendelea kusikiliza dhihaka kutoka kwa Ojuku, alichokifanya ni kukata simu.
Alichanganyikiwa, kwa tukio lililotokea, hakuamini kama Usalama wa Taifa walishindwa kugundua mahali ndege hiyo ilipokuwa. Mawasiliano yalifanyika kutoka katika uwanja wa ndege mmoja mpaka mwingine lakini cha ajabu hakukuwa na taarifa zozote ambazo zilisema mahali ndege hiyo ilipokuwa.
Wakenya walishangaa, hawakuamini kile kilichotokea, ilikuwaje ndege ya rais wao ipotee katika mazingira ya kutatanisha? Taarifa mbalimbali zilizokuwa zikiandikwa katika Akaunti ya Mabadiliko ya Kweli kwenye Mtandao wa Kijamii wa Instagram zilionyesha kabisa mtu aliyekuwa akiandika posti hizo alijua mahali ndege hiyo ilipokuwa.
Hakutaka kupoteza muda, hapohapo akampigia simu Olotu kwa lengo la kumwambia kile kilichokuwa kimetokea. Wala hazikupita sekunde nyingi simu ikapokelewa.
“Nilitaka nikupigie. Niambie kiongozi,” alisikika Olotu kwenye simu.
“Umeona kilichotokea?” aliuliza Rais Onyango.
“Nimeona! Nimechanganyikiwa. Ndege imekwenda wapi?” aliuliza Olotu huku kwa kuisikia sauti yake tu halikuwa jambo gumu kugundua kwamba alikuwa amechanganyikiwa.
“Hata sisi hatujui! Ila mkuu wa majeshi nchini Tanzania anajua mahali ndege ilipo,” alisema Olotu huku akionekana kuwa na uhakika.
Taarifa hizo ziliendelea kuwashangaza kila watu duniani, lilikuwa jambo lisilowezekana hata kidogo kwa ndege ya rais yeyote kupotea katika mazingira ya kutatanisha. Simu zilipigwa katika viwanja vyote vikubwa, hawakuwa na taarifa juu ya ndege hiyo, kila sehemu walisema kwamba ndege haikuwa imeonekana.
“Kwa hiyo imepotea kama ndege ya Malaysia?” alihoji mwandishi wa kituo cha Televisheni cha NBC nchini Kenya.
“Hakuna anayjua, Usalama wa Taifa hawazungumzi kitu chochote kile, nahisi katika hili kuna mtu ndani ya serikali anajua kinachoendelea,” alisema mwandishi mwingine.
Kila mmoja alijua kabisa kwamba Tanzania ilikuwa ikijua mahali ndege ilipokuwa, maneno kwenye mitandao ya kijamii yalikuwa yakiwachanganya Wakenya lakini wengi wao walikuwa wakiuamini ukurasa wa Mabadiliko ya Kweli ambao kwa kipindi hicho ulizidi kushika kiki mpaka kufikisha wafuasi milioni sabini huku Wakenya nao wakiwa wengi kuufuatilia.
“Ndege ipo Afrika, nchi fulani hivi! Ila kwa sababu ilitumika vibaya, itafunguliwa yote na itakwenda kuundwa katika nchi moja huko Asia, itauza huko na pesa kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu nchini Kenya. Hiyo itakuwa fundisho kwa serikali nyingine za Afrika ambazo zinaifanya ndege ya rais kuingia katika kazi nyingine ambayo haikupaswa kuingia. Hayo ni matumizi mabaya ya serikali,” aliandika Godwin katika akaunti ile kitu kilichowafanya watu wengi kutokuwa na uhakika kama ndege itapatikana.
“Hebu tuambie ukweli! Kwa hiyo ndege haitoonekana?” aliuliza jamaa mmoja kwenye posti hiyo.
“Ndiyo! Hivi ninavyoongea, ndiyo inafunguliwa yote na vifaa vyake kusafirishwa,” alijibu Godwin kisha kutuma emoj ya mtu anayecheka sana.
Serikali ya Kenya ikachafuka, hakukuwa na mtu aliyeamini kama kitu hicho kilifanyika katika nchi hiyo ambayo iliaminika kuwa na ulinzi wa hali ya juu. Walijua kwamba ndege hiyo ilikuwa sehemu fulani lakini kitu cha ajabu kabisa walipiga simu katika nchi zote za Afrika na kuambiwa kwamba ndege hiyo haikuwepo katika nchi hizo.
“Burundi, Kongo, Namibia, Senegal, Nigeria na nchi zote tumepiga simu na kuambiwa kwamba ndege hiyo haipo,” alisema waziri mkuu wa nchi hiyo.
“Tanzania! Itakuwa katika Uwanja wa Ndege wa JFK, tuma watu waende Tanzania,” aliagiza Rais Onyango huku akionekana kuchanganyikiwa zaidi.
Hakukuwa na muda wa kupoteza, haraka sana Usalama wa Taifa wakatumwa huko huku baadhi ambao walijifanya kuwa kama wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakitangulia katika uwanja huo kwa ajili ya kuchunguza kama kulikuwa na ndege hiyo.
Walipofika huko, haraka sana wakaanza kufanya uchunguzi. Lilikuwa jambo gumu mno kuipata, hakukuwa na mtu aliyekuwa akijua kama ndege hiyo ilikuwa nchini Kongo na wakati huo ilikuwa ikifunguliwa kwa ajili ya vifaa vyake kusafirishwa kwenda kuuzwa nchini Japan.
Walichunguza kwa siri, tena kwa kila eneo lakini hawakuweza kuiona ndege hiyo kitu kilichomchanganya zaidi Rais Onyango.
“Huu ni uadui! Hatuwezi kukubali aibu hii! Lazima tuivamie nchi yako,” alisema Onyango kwenye simu, alikuwa akizungumza na Ojuku.
“Kisa?”
“Ndege yetu ipo wapi?”
“Kwani nani kaichukua?”
“Tuambieni ndege yetu ipo wapi?”
“Hatujui! Kwa kuwa suala hilo ulilipata katika mitandao ya kijamii, hebu nenda kaulize hukohuko, wanaweza kukupa majibu,” alisema Ojuku na kukata simu.
Wakati hayo yakiendelea, ndege hiyo ilikuwa ikifunguliwa, ilikuwa ni lazima isafirishwe, hayo yalikuwa maagizo ya Godwin, alikuwa na hasira, alipompa Ojuku maagizo hayo, hakupinga bali alikubaliana naye kwani kwa kipindi hicho ukimzungumzia Godwin, ilionekana kama unamzungumzia malaika aliyetumwa kuilinda nchi hiyo.
Yeye mwenyewe akafanya mawasiliano na rafiki yake aliyekuwa nchini Japan, Yokoshima Inamoto ambaye alisoma naye, katika kipindi hicho alikuwa akifanya kazi ya udalali katika mitandao mbalimbali ikiwemo Alibaba, Amazon na mitandao mingine mingi duniani.
Akamwambia kwamba kulikuwa na mzigo alitaka kumpelekea kwa ajili ya kuuza kwa matajiri waliokuwa wakitaka, alipouliza, akajibiwa kwamba ilikuwa ndege ya Rais wa Kenya ambayo ilikuwa ikitafutwa kila kona.
“Hakuna shida. Mmekwishaitenganisha?” aliuliza Inamoto.
“Ndiyo kazi hiyo inafanyika, ikiwa tayari, tutaituma huko kwa kutumia meli yetu, itafungwa katika makontena,” alisema Godwin.
“Sawa. Iwe kiasi gani?”
“Dola bilioni nne.”
“Nitaiuza kwa dola bilioni tano, moja ya dalali hapa,” alisema Inamoto kijana aliyejua kutafuta pesa kupitia mali za watu.
“Haina shida.”


Ojuku aliwasiliana na rais wa Kongo, Bwana Boniphace Kaposhoo na kumwambia kuhusu ndege ambayo ilitakiwa kusafirishwa haraka sana kuelekea nchini mwake. Hilo lilikuwa jambo gumu sana kukubali, alikataa lakini kutokana na maneno matamu aliyoyatumia mwanaume huyo, mwisho wa siku Kaposhoo akakubaliana naye ila kwa sharti kwamba ndege hiyo haikutakiwa kutua katika Uwanja wa Kimataifa wa Kinshasa bali ilitakiwa kupelekwa Bumba.
Hilo halikuwa tatizo, Ojuku akamwambia Godwin ambaye aliwapigia simu marubani na kuwaambia ni kitu gani kilitakiwa kufanyika wakati huo. Kila kitu kilikamilika na hiyo kuitwa wataalamu wa kuifungua ndege na kuanza kufanya kazi yao ambayo iliwachukua saa sita, ilipokamilika, wakaipakiza katika lori lililokuwa mahali hapo na kuondoka kuelekea nchini Tanzania kupitia mkoani Kigoma huku likiwa chini ya ulinzi wa wanajeshi.
Wakati hayo yakiendelea, Wilson, Okotee na marubani walichukuliwa, wakaingizwa ndani ya gari na wao kuanza kusafirishwa kuelekea nchini Tanzania. Kila mmoja aliogopa, walijua kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wao kwani kwa jinsi wanajeshi wale walivyoonekana, walionekana kutokuwa na masihara hata kidogo.
Baada ya saa chache wakafika mkoani Kigoma ambapo hapom wakapandishwa ndege na kupelekwa nchini Tanzania wakiwa na Bokasa ambaye alikuwa akitafutwa kwa udi na uvumba.
“Mkuu! Tutakuwa huko ndani ya saa chache, ndiyo tunaondoka Kigoma,” alisema mkuu wa kikosi cha Leopard ambao walikwenda nchini Kongo kwa ajili ya kufanya oparesheni waliyokuwa wamepewa.
Bokasa alikuwa kimya, moyo wake ulijisikia uchungu mno, hakuamini kama kweli alikuwa amepatikana kizembe na kupelekwa nchini Tanzania. Aliamini kwamba kama angeendelea kukaa Ubelgiji basi maisha yake yangekuwa na amani na hata Watanzania waliokuwa wakimtafuta wangesubiri mpaka miezi sita ipite ndiyo wamsafirishe kwa kuwa tu waliheshimu maamuzi ya madaktari.
Kwa kutumia ndege ya kijeshi, walichukua saa moja tu wakafika jijini Dar es Salaam ambapo wakachukuliwa na kuingizwa ndani ya gari na kuondolewa mahali hapo. Hakukuwa na mtu aliyekuwa akijua juu ya uwepo wa Bokasa nchini Tanzania, alipelekwa kimyakimya na kuondolewa mahali hapo hivyohivyo.
Hakukuwa na waandishi wa habari, tukio hilo lilikuwa la siri sana kwani waliamini kama Wakenya wangejua basi wangekuwa na uhakika kwamba Tanzania ndiyo iliyofanya mpaka ndege hiyo kupotea katika mazingira ya kutatanisha.
“Tufanyeje ili wasijue kwani ni lazima Bokasa apandishwe mahakamani!” alisema Meja Jenerali.
“Bado sijajua! Hapa tunatakiwa kufanya kitu kimoja cha hatari sana. Au tuseme kwamba ndege ilitekwa na watu halafu tukaiokoa na kumchukua mtu wetu?” aliuliza Ojuku.
“Hapana! Watauliza hiyo ndege ipo wapi waifuatilie!”
“Basi tuseme kwamba ililipuka!”
“Watauliza Bokasa kaponaje!”
“Kwa hiyo tufanye nini?”
“Sijui! Labda tuendelee kujifikiria zaidi!”
“Subiri! Nadhani Godwin anajua nini cha kufanya, ngoja nimpigie simu,” alisema Ojuku, hakutaka kumaliza, hapohapo akampigia simu Godwin kwa ajili ya kuzungumza naye.
Alimwambia wazi kwamba akili yao ilifika mwisho, hawakujua ni kitu gani walitakiwa kufanya ili watoke katika tukio hilo la kuhisiwa kwamba wao ndiyo walifanya kila liwezekanalo kuhakikisha ndege hiyo inapotezwa.
“Ni kazi rahisi sana!” alisema Godwin.
“Ndiyo maana nimekupigia simu! Tufanye nini?”
“Kuna msemo mmoja wa Kiingereza unasema hivi; ‘Enemy of my friend is enemy of mine’ ukimaanisha kwamba adui wa rafiki yangu ni adui wangu pia’” alisema Godwin.
“Unamaanisha nini?”
“Ngoja nifanye jambo moja! Wewe sikiliza kitakachotokea Kenya. Hakuna atakayejua kama Tanzania imehusika katika tukio hili. Nataka washikane uchawi wao kwa wao,” alisema Godwin.
“Utafanya nini?”
“Subiri! Tega masikio utasikia kitakachotokea huko,” alisema Godwin na kukata simu. Macho na masikio ya Ojuku yakawa nchini Kenya, akataka kuona ni kitu gani ambacho Godwin angefanya mpaka watu hao kushikana uchawi wao kwa wao.

Je, nini kitaendelea?

Kwa kawaida huwa siombi muhtasari…

wacha ujinga umbwa hii! sisi kama Villagers hatugwes kaa chini tusome hai upus!

:meffi::meffi:

Summarize!

mtu alete summary