Very well written report in Kiswahili about S.A.

Vurugu Afrika Kusini.

Walengwa wakuu walikuwa Wanigeria, Wasomalia, Wachina, Watanzania 21 wakubali kurejeshwa nchini, wanaishi kambini.

Wakati serikali ikitangaza kuwarejesha Watanzania 21 kati ya 23 walioko kwenye moja ya makambi yanayowahifadhi raia wa kigeni walioathirika na vurugu zilizohusisha mauaji, uporaji na watu kukimbia makazi nchini Afrika Kusini, Mtanzania aliyeko nchini humo, amesimulia jinsi raia wengi wa kigeni walivyoathirika.

Joseph Moses, anayeishi mjini Durban, amesema pamoja na baadhi ya raia wa kigeni kuawa, lakini waliothirika hadi sasa wengi wao hawajui watalipwaje mali zao zilizopotea katika ghasia hizo.

Moses, ambaye alizungumza na NIPASHE kutoka nchini humo jana, alisema kuna Watanzania wengi mjini Durban wamepoteza mali zao katika vurugu hizo na hawajui watalipwaje.

Hata hivyo, alisema raia wa kigeni walioathirika zaidi na ghasia hizo ni wanaotoka katika nchi za China, Pakistan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Nigeria na Somalia, baada ya maduka pamoja na nyumba wanazoishi kuvamiwa na watu wanaosaidikiwa kuwa ni raia wa Afrika Kusini na kuporwa.
“Kinacholeta utata ni kwamba, hata kama fidia itatolewa haijulikani itakuwaje,” alisema Moses na kuongeza kuwa kuna idadi kubwa ya Watanzania wanaoishi katika mji wa Durban ambao umeathiriwa zaidi na vurugu hizo.

Alisema jana ulifanyika mkutano uliomhusisha Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, Chifu wa Wazulu, Goodwill Zweluthini anayetuhumiwa kuchochea vurugu hizo na viongozi wengine nchini humo katika kambi ya waathirika hao mjini Durban.

Moses alisema katika mkutano huo, Chifu Zweluthini aliwapiga marufuku raia wa Afrika Kusini kuendelea kuwashambulia raia wa kigeni.

Alisema sababu iliyotolewa na Chifu Zweluthini ni kwamba, nchi nyingi za Afrika, ikiwamo Tanzania, ziliwasaidia weusi wa nchi hiyo kuondoa siasa ya ubaguzi wa rangi.

Hata hivyo, alisema hakuna Mtanzania aliyeuawa katika vurugu hizo zilizosababisha mauaji ya raia wanane wa kigeni.

WATANZANIA 21 KUREJESHWA NCHINI
Wakati Moses akisema hayo, Watanzania 21 kati ya 23 walioko kwenye kambi hiyo wamekubali kurejea nchini baada ya serikali kuwahakikishia kuwalipia gharama za safari, lakini wawili wamekataa.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa, Watanzania wanaoishi Afrika Kusini wanakisiwa kuwa zaidi ya 10,000.

Alisema kati yao, 23 ndio waliobainika kuhifadhiwa katika kambi hiyo kufuatia kuibuka kwa ghasia hizo nchini humo.

Kutokana na hali hiyo, alisema serikali imekubali kugharimia safari ya Watanzania hao 21 baada ya wenyewe kukubali kurejea nchini.

Alisema Watanzania hao 21 ni miongoni mwa raia wa kigeni ambao baadhi wanasadikiwa kupoteza kazi na wengine shughuli zao za biashara kuharibiwa katika ghasia hizo.

Ghasia hizo ziliibuka wiki iliyopita mjini Durban na kuenea katika miji mingine ya Johannesburg na Alexandria, nchini humo.

Alisema maofisa wa Tanzania kwa kushirikiana na ubalozi nchini Afrika Kusini wanafanya uchunguzi ili kubaini Watanzania hao kila mmoja alichopoteza, ikiwamo kazi na biashara katika ghasia hizo.

Waziri Membe alisema iwapo itabainika kuna walichopoteza, serikali za nchi hizo zitaangalia nini la kufanya kuwasaidia.

Alisema hadi sasa vurugu hizo zilizoibuka baada ya mmoja wa walinzi ambaye ni raia wa kigeni katika duka moja kubwa Afrika Kusini kumuua kwa risasi raia wa nchi hiyo wiki iliyopita, zimesababisha takriban raia nane wa kigeni wanaotoka katika nchi za Ethiopia, Zimbabwe, Malawi na Swaziland.

Hata hivyo, Membe alisema hakuna Mtanzania anayeishi nchini humo aliyeuawa katika vurugu hizo na kwamba watu watatu wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya raia wa Msumbiji wamekamatwa katika msako mkali unaoendelea nchini Afrika Kusini.

“Nimezungumza na Waziri wa Usalama wa Afrika Kusini, balozi, wenzetu wa Zimbabwe, Mwenyekiti wa Sadc (Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika), tumepeleka wenzetu wa Durban, swali kubwa je, tumepoteza Watanzania wangapi? Hatujapoteza Mtanzania hata mmoja katika mgogoro huo,” alisema Waziri Membe.

Aliongeza: “Nimekutana na Balozi wa Afrika Kusini leo (jana) kumueleza masikitiko ya Tanzania na kumtaka kuhakikisha Watanzania walioko Afrika Kusini wanakuwa salama.”

Hata hivyo, alisema kuna Watanzania watatu waliokufa katika matukio mengine matatu tofauti, ambayo hayahusiani na vurugu hizo.

Aliwataja Watanzania hao kuwa ni Athuman Mapepe, aliyekufa baada ya kuchomwa kisu na wafungwa wenzake gerezani, Rashid Jumanne, aliyeuawa kilomita 90 kutoka mjini Durban akiwa kwenye kitendo cha unyang’anyi na Ally Heshima aliyefia hospitali jijini Johannesburg kwa maradhi ya kifua kikuu na kwamba mwili wake ulirejeshwa nchini juzi.

Alisema Tanzania inaungana na Umoja wa Afrika (AU) kupitia mwenyekiti wake, ambaye ni Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, pamoja na Sadc kulaani vitendo vyote viovu walivyofanyiwa raia wa kigeni nchini Afrika Kusini katika vurugu hizo, kwani ni kinyume cha haki za binadamu

KAULI YA CUF
Katika hatua nyingine, Chama cha Wananchi (CUF) kimesema kinasikitishwa na machafuko yanayoendelea nchini Afrika Kusini dhidi ya wakazi wasio wenyeji wa nchi hiyo, wakiwamo Watanzania.

“Haingii akilini hata kidogo baada ya muda mrefu kupambana na makaburu kusaka uhuru wa Afrika leo hii waafrika tunaanza kufukuzana wenyewe,” alisema Naibu Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CUF, Abdallah Mtolea.

Aliongeza: “Ni wakati, ambao Waafrika Kusini wanapaswa kujua kuwa si wao wanaopoteza ajira tu kwa kuwapo wageni nchini kwao, bali hata mataifa mengine kama Tanzania pia ajira za raia wake zinapotea kwa kuwapo wageni kutoka Afrika Kusini lakini tunavumiliana na hivyo ndivyo tunapaswa kuishi.”

Aliitaka serikali ya Afrika Kusini kuongeza nguvu na kuharakisha kukomesha vitendo vya kibaguzi, hasa kwa wageni wanaotoka nje ya nchi hiyo.

Alisema kwa mujibu wa vyombo vya habari, Chifu Zweluthini amekuwa miongoni mwa wachochezi wa kushambuliwa na kufukuzwa wageni nchini humo.

“Ni wajibu wa serikali ya Afrika Kusini kumwajibisha kisheria ili matendo haya yasiendelee.

Tukizuia isitokee Afrika Kusini tutakuwa tumesaidia hali kama hii isitokee nchi nyingine za Afrika,” alisema Mtolea.

Alisema CUF ina taarifa kuwa Watanzania walioko Afrika Kusini ni miongoni mwa waliojeruhiwa na kufanyiwa vurugu.

“Kuna fununu ya Watanzania wawili kufariki dunia. Tunaitaka serikali ya Tanzania kupitia ubalozi wake nchini Afrika Kusini kuthibitisha hili ili kuondoa wasiwasi,” alisema Mtolea.

Aliongeza: “CUF tunajua ni wajibu wa kila Mtanzania kumlinda Mtanzania mwenzake. Na ni wajibu wa serikali kulinda raia wake popote pale walipo duniani. Serikali ya Tanzania haionyeshi kama inawashughulikia Watanznaia walioko Afrika Kusini. Tunaitaka serikali kubeba jukumu la kuwarudisha nyumbani mara moja Watanzania walioko hatarini nchini Afrika Kusini.”
CHANZO: NIPASHE

This is a complete report. Very well written.
http://www.mtanzaniaforums.com/index.php/component/k2/itemlist/date/2015/4/21

Teacher Ndauwo bado hujapigwa transfer kutoka ole kundu primary school?

hii ni ile kiswahili ya mandauo wa TZ

1 Like

NDAUWO NI NDAUWO TUUUUU SCHUPIT

Summarise…:mad::mad:

Yenyewe kusoma na kukompriendi kiswahili ni kigumu